NA DIRAMAKINI
KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam imefungua ukurasa mpya katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya kujikusanyia alama tatu zikisindikizwa na mabao matatu.
Ni baada ya kumenyana na Tabora United katika mtanange uliopigwa leo Agosti 18,2024 katika dimba la KMC Complex lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Aliyeanza na nyota njema kwa msimu wa Ligi Kuu ya 2024/25 katika klabu ya Simba SC dhidi ya Tabora United ni mlinzi wa kati Che Fondoh Malone ambaye alifunga bao la kwanza dakika ya 13 kwa kichwa.
Che Fondoh Malone alimalizia mpira uliopigwa na Jean Charles Ahoua, ambapo walionekana kuutawala vema mchezo huo.
Katika kipindi cha pili, Valentino Mashaka aliwapatia bao la pili dakika ya 68 kwa kichwa baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’.
Awesu Awesu aliwapatia Simba SC bao la tatu dakika ya 90' akiwa ndani ya 18 kufuatia mpira wa krosi uliopigwa na Kibu Denis kuokolewa na walinzi wa Tabora United.
Mchezaji huyo wa zamani wa KMC aliandikisha bao lake la kwanza kwa Wekundu hao baada ya kukamilisha dili lake siku ya mwisho ya dirisha la uhamisho.
Hata hivyo, Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Joshua Mutale alishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 31 baada ya kupata maumivu ya mguu.
Tags
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania
Habari
Ligi Kuu ya NBC
Michezo
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
Simba SC
Tabora United FC