ZANZIBAR-Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Mheshimiwa Lela Muhamed Mussa amaesema, Serikali itaendelea kutafuta fursa mbalimbali za kuwawezesha wananchi kujiajiri ili kupunguza changamoto ya ajira nchini.
Ameyasema hayo katika ukumbi wa wizara hiyo Mazizini, mara baada ya kushuhudia utiaji wa saini Hati ya Makubaliano (MOU) ya utekelezaji wa Mradi wa Uchumi wa Buluu, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.
Mradi huo unatatekelezwa kwa mashirikiano baina ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali (Vocational Training Authority) na Wakala wa Maendeleo wa Ubelgiji (Belgium Develepment Agency-Enable).
Amesema, mradi huo unaolenga kuwapatia mafunzo vijana wa vyuo vya amali utasaidia vijana hao kujiajiri baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo.
Mapema Waziri Lela aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa kufadhili mradi huo pamoja na Wakala wa Maendeleo wa Ubelgiji (Belgium Develepment Agency-Enable) kwa kuiamini wizara hiyo na kuingia makubaliano ya kuendesha mafunzo hayo yatakayosaidia kupunguza vijana wasio na kazi nchini.
Hata hivyo, amewaomba wadau hao kuanzisha mradi mwingine wa kuwaunganisha na masoko ya kuuza bidhaa na ajira kwa vijana watakaobahatika kupatiwa mafunzo hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali, Dkt. Bakar Ali Silima amesema, mradi huo utatekelezwa katika Chuo cha Amali Daya na Vitongoji Pemba, ambapo vijana 320 watapatiwa mafunzo katika Sekta ya Uvuvi, Gesi na Uhunzi.
Aidha, amesema mradi huo umejikita kuwasomesha wafanyakazi wa vyuo hivyo na kuwapatia vifaa vya karakakana na vitendea kazi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mkurugenzi Wakala wa Maendeleo wa Ubelgiji (Belgium Develepment Agency-Enable),Koen Goekint amesema, mradi huo wa miaka mitatu umelenga kuwawezesha vijana kujiajiri ambapo kiasi cha shilingi milioni 720 zitatumika na kuzalisha ajira zaidi ya 3,000 wakati wa mradi huo.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali, Dkt. Bakar Ali Silima na Mkurugenzi Wakala wa Maendeleo wa Ubelgiji (Belgium Develepment Agency-Enable),Koen Goekint.