SUA,MWEKA na UDSM wajengewa uwezo kutafiti kuhusu viumbe hai vilivyo hatarini kutoweka

MOROGORO-Wanafunzi pamoja na Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), MWEKA pamoja na UDSM wamejengewa uwezo wa kufanya tafiti za kutambua viumbe hai vilivyo karibuni kutoweka.
Sambamba na kupatiwa vifaa vya kitaalamu vitakavyowawezesha kupima na kuhifadhi sampuli za viumbe hai hivyo kupitia mradi wa CONTAN unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

Akizungumza kwenye kongamano la wadau, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala-SUA, Prof. Amandus Muhairwa amesema, SUA ni moja ya vyuo vilivyonufaika na mradi huo katika kujengewa uwezo na kupata vifaa vya kupima na kuhifadhi sampuli.
"Mafanikio makubwa tuliyoyapata SUA, kuwezesha walimu wetu kufundishwa kuhusu viumbe hai kiwango cha kimataifa na kupata vifaa vya kufundishia ikiwemo hadubini,"amesema Prof. Muhairwa.

Dkt. Charles Kilawe ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo pia ni mmoja wa waratibu wa mradi wa CONTAN amesema,, CONTAN ni mradi wa miaka minne ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2021.
Ni katika vyuo vya SUA, UDSM na MWECAU ukiwa na lengo la kuwezesha wanafunzi na kujengewa uwezo wa kutambua baionuai ambazo zipo hatarini kutoweka na namna ya kuzilinda kwa kushirikiana na wahifadhi wa wanyamapori na wahifadhi wa misitu.

"Kupitia mradi huo tumeweza kununua hadubini za kisasa ambazo kwa hapa nchini unaweza kuzipata MWECAU na hapa SUA tu, pia tumenunua vifaa vingine kama jenereta, makabati ya kuhifadhia sampuli kavu za mimea na wadudu ambazo zinatumika katika kufanya tafiti mbalimbali,"amesema Dkt. Kilawe.

Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Odzungwa, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Theodora Aloye amesema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa katika jamii katika kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kuhifadhi wa viumbe hai vilivyo hatarini kutoweka."Kupitia mradi wa CONTAN jamii imeweza kunufaika kwa kiasi kikubwa kwani kipindi mradi unaendelea wanakijiji walio pembezoni mwa hifadhi yetu ya milima ya Odzungwa walikuwa wananufaika kwa kupata ajira za muda mfupi na kupata kipato, kwani wanafunzi walikuwa wanakuja kufanya mafunzo.

"Kila wanafunzi wanapokuja mafunzo kwa vitendo tulikuwa tunachukua wanakijiji kwa ajili ya kuaanda mazingira, hivyo walikuwa wanapata ajira kwa kushiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kukusanya sampuli za mimea na wadudu,"amesema Mkuu wa Hifadhi Odzungwa.
Amesema, hifadhi ya milima ya Odzungwa imechaguliwa kuwa moja ya sehemu ya wanafunzi kuweza kujifunzi kupitia mradi wa CONTAN kutokana na upekee wake, ikiwemo kuwepo kwa msitu uliohifadhi kwa umahiri mkubwa na kupabwa na aina mbalimbali ya mimea, wadudu na wanyamapori.

Hadija Mchelu ni Mkufunzi msaidizi Idara ya Utunzaji na usimamizi wa mifumo Ikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mmoja wa wanafunzi walionufaika na mradi wa CONTAN amesema kupitia mradi wameweza kujengewa uwezo utakaowasaidia kufanya tafiti na kubaini viumbe hai na kuzihifadhi.
"Kama mwanafunzi niliweza kusoma kozi mbalimbali ikiwemo kujifunzi namna ya kukusanya taarifa za viumbe hai (biodiversity monitoring data collections) ambazo zitatusaidia katika kufanya tafiti na kuandaa machapisho ya kisayansi.

"Pia ujuzi ambao nimeupata kupitia huu mradi umenisaidia mimi kuandika machapisho ya kisayansi ambayo nimeweza kuyatengeneza kwa urahisi zaidi ukilinganisha na hapo awali nilivyokuwa sijapata ujuzi tunawashukuru sana,"ameongeza Hadija.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news