MORONI-Taasisi za fedha za Tanzania zinazoshiriki kliniki ya Diaspora mjini Moroni, Comoro tarehe 5 Agosti, 2024 zimemtembelea Benki Kuu ya Comoro kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa sekta ya fedha ya Comoro.
Ujumbe wa taasisi hizo ulioongozwa na Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Said Yakubu ulikutana na kufanya majadiliano na Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo, Dkt. Younoussa Imani.
Katika majadiliano hayo, Dkt. Imani aliwaeleza namna Diaspora wa Comoro wanavyotuma fedha kwa wingi nchini humo. Alisema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kiwango cha fedha kinachotumwa na diaspora ni takribani mara tatu ya bajeti ya mwaka ya nchi hiyo na fedha zote hizo zinaingia katika mzunguko kwa ajili ya matumizi.
Aliongeza kuwa mpango wa Serikali yao kwa sasa ni kushawishi fedha hizo zielekezwe zaidi kwenye uwekezaji na kuzikaribisha benki za Tanzania kuwekeza nchini humo.