TEA na TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd zajadili ushirikiano katika miradi ya elimu

DODOMA-Wawakilishi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd wamekutana kwa lengo la kuona namna wanavyoweza kutekeleza kwa ushirikiano miradi ya kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia hapa nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA, CPA Mwanahamisi Chambega (kushoto) na Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano wa Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd, Bi.Getrude Mpangile (kulia) katika kikao cha kujadili ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya elimu baina yao.

Mkutano huo umefanyika Agosti 27,2024 makao makuu ya TEA, Ilazo jijini Dodoma na kuongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA, CPA Mwanahamisi Chambega ambapo amesema TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd imekuwa mdau wa TEA wa siku nyingi na kwamba TEA iko tayari kuendelea kushirikiana nao.
Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano wa Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd, Bi. Getrude Mpangile (kushoto) na Meneja Mawasiliano wa TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd, Bi. Anita Bulindi wakishiriki kikao cha kujadili ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya elimu baina yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano wa Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd, Bi. Getrude Mpangile amesema, katika mwaka huu kampuni hiyo imetengeneza madawati 200 yenye thamani ya shilingi milioni 25.9 ambayo yatanufaisha wanafunzi 600 katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Tayari madawati 70 yamepelekwa katika Shule ya Msingi Makuburi ya Dar es Salaam yakinufaisha wanafunzi 210 ambapo madawati mengine 130 yatapelekwa katika shule za Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani na kunufaisha wanafunzi 390.
Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya TEA walioshiriki kikao cha pamoja na Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd kujadili ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya elimu baina yao.

Bi.Mpangile ameongeza kuwa, mradi mwingine unaotekelezwa na TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd katika mwaka huu ni ule wa kuwezesha wanafunzi wa kike mashuleni ukijikita katika kutoa taulo za kike.

Jumla ya katoni 500 zenye thamani ya shilingi milioni 35.4 zimelengwa kusambazwa kupitia mradi huo wa taulo za kike. Tayari katoni 75 zimesambazwa kwa wanafunzi wanufaika 2000 katika mikoa ya Pwani na Songwe.
Watumishi wa TEA walioshiriki kikao cha pamoja na kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd kujadili ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya elimu baina yao.

Aidha, TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd inajihusisha na utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi katika Mkoa wa Dar es Salaam ukienda sanjari na utunzaji wa mazingira kwa kuhamasisha upandaji miti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news