NA DIRAMAKINI
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa chini ya miaka 21 (France U-23), Thierry Henry amejiuzulu huku taarifa ya Fédération Française de Football (FFF) ikitaja uamuzi huo ameufikia kwa sababu zake binafsi.
Thierry Henry amejiuzulu ukocha France U-23.(Picha na Getty Images).
Aidha, hayo yanajiri baada ya kocha huyo kuongoza timu hiyo kutwaa Medali ya Fedha katika mashindano ya Olimpiki 2024 yaliyohitimika hivi karibuni nchini Ufaransa.
Thierry Henry alipewa jukumu la kuiongoza timu hiyo Agosti 2023, akichukua nafasi ya Sylvain Riopun na alikuwa ametia saini mkataba wa miaka miwili hadi 2025.
Kupitia taarifa ya FFF, Thierry Henry alieleza kuwa, "Ningependa kuwashukuru FFF na rais (wa shirikisho) Philippe Diallo, ambao walinipa fursa hii nzuri.
"Kushinda Medali ya Fedha katika Michezo ya Olimpiki kwa nchi yangu kutasalia kuwa moja ya fahari kubwa maishani mwangu. Ninashukuru sana shirikisho, wachezaji, wafanyakazi na mashabiki walioniruhusu kuonesha uzoefu wangu." (NA)