TMA yatangaza mvua za Vuli mwezi Oktoba hadi Desemba,2024

DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za Vuli, 2024 zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu ambazo zitakuwa chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi pamoja na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 21, 2024 jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema kuwa, mvua za vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024.

Ni katika ukanda wa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, mwaka huu.

Dkt. Chang’a amesema kuwa mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2024, huku kukitarajiwa kuwa na vipindi vya joto kali kuliko kawaida katika msimu wa vuli.

“Uwepo wa La-Niña hafifu unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu wa vuli, 2024, athari zinazotarajiwa ni upungufu wa unyevunyevu katika udongo katika maeneo mengi na hivyo kuathiri shughuli za kilimo,” amesema Dkt. Chang’a.

Amesema kuwa,kina cha maji katika mito na mabwawa vinatarajiwa kupungua pamoja na kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama.

Dkt. Chang’a amesema kuwa,mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).

Pia Ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Dkt. Chang’a ametoa wito kwa sekta mbalimbali nchini kuchukua tahadhari ikiwemo sekta ya kilimo kwani kutakuwa na upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi.

“Hali hii inatarajiwa kuathiri ukuaji wa mazao, wadudu na magonjwa ya mazao yanatarajiwa kuongezeka katika msimu hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao, upatikanaji wa mazao ya misitu kama vile asali kutokana na uhaba wa maji na maua,” amesema Dkt. Chang’a.

Amesema kuwa,wakulima wanashauriwa kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo, kuandaa mashamba kwa wakati, kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame.

Dkt. Chang’a amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kufuatilia na kupata taarifa sahihi za utabiri na tahadhari ya Hali ya hewa kutoka TMA na kuzisambaza kwa wakati ili kuelimisha umma na kuepuka athari zinazoweza kujitokeza pamoja na wananchi kufatilia taarifa za Hali ya hewa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news