TMA yawataka wakulima kujiandaa kuepuka hasara mvua za Vuli

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa, kipindi cha msimu wa mvua za Vuli, upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua hizo nchini.

Miongoni mwa maeneo hayo ni Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Ukanda wa Pwani ya Kaskazini.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a ameyasema hayo leo Agosti 22,2024 jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari wakati akiwasilisha taarifa kuelekea mvua za Vuli mwezi Oktoba hadi Desemba,2024.

Utabiri huo ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikihusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba.

Pia,Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Kaskazini mwa Kigoma

Dkt.Chang’a amesema, hali hiyo inatarajiwa kuathiri ukuaji wa mazao huku wadudu na magonjwa ya mazao yakitarajiwa kuongezeka katika msimu, hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao.

Amesema, upatikanaji wa mazao ya misitu kama vile asali unatarajiwa kuathirika kutokana na uhaba wa maji na maua.

"Wakulima wanashauriwa kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo."

Aidha, wanashauriwa kuandaa mashamba kwa wakati, kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame. 

Pia, wakulima wanashauriwa kupanda mazao tofauti tofauti yanayostahimili ukame ili kupunguza madhara yatakayoweza kujitokeza endapo zao moja litaathirika. 

"Halikadhalika, mamlaka husika zinashauriwa kutoa elimu na uelewa kwa wakulima juu ya njia bora na namna ya kutumia kiwango kidogo cha mvua kinachotarajiwa pamoja na matumizi mazuri ya akiba ya chakula kilichopo. 

"Wakulima pia wanahimizwa kupata ushauri kutoka kwa maafisa ugani kuhusu namna bora ya kuendesha shughuli za kilimo,"ameongeza Dkt.Chang’a.

Msimu wa mvua za vuli mahususi zitakuwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ikijumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, na Kilimanjaro, Pwani ya Kaskazini, Kaskazini ya Mkoa wa Morogoro.

Mikoa ya Pwani ikijumuisha Visiwa vya Mafia, Dar es salaam, Tanga na mikoa ya Ukanda wa Ziwa Victoria.

Dkt.Chang’a amebainisha kuwa, Kanda ya Ziwa Victoria mvua za mvuli zinatarajiwa kuwa wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ambapo zitaanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024 katika mikoa ya Geita.

Kagera na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na kutawanyika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2024.

Amesema kuwa,mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Desemba, 2024.

Vile vile amesema, mvua za vuli za wastani maeneo ya Pwani, Morogoro, Visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga na Visiwa vya Unguja na Pemba zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Desemba, 2024.

Aidha, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ambayo ni mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kutakuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani kuanzia wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Desemba, 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news