TRA Sikia App yazinduliwa

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua programu tumishi ya TRA Sikia App ambayo ili kupokea maoni na malalamiko ya wafanyabiashara nchini, dhamira ikiwa ni kuboresha huduma za mamlaka hiyo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),CPA Yussuf Mwenda akizungumza na wahariri na wanahabari (hawapo pichani) Agosti 9,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuzindua TRA Sikia App.

Uzinduzi huo umefanywa Agosti 9,2024 na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo,CPA Yussuf Mwenda jijini Dar es Salaam.

CPA Mwenda amesema,katika kutatua migogoro ya wafanyabiashara wakiwemo wa Kariakoo, mamlaka imeweka utaratibu wa kukutana nao mara tatu kwa mwezi ili kuwasikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero zinazowakabili.

Pia,CPA Mwenda amesema kupitia programu tumishi hiyo,malalamiko, maoni na ushauri ambao utatumwa iwe na mfanyabiashara au mwananchi popote alipo utamfikia Kamishna Mkuu moja kwa moja.

“Tutakutana nao kwa mwezi mara tatu na mimi nitakuwa ninakwenda kukutana nao ili kutatua matatizo yao na ndilo la msingi zaidi. Tunafanya hivyo."

Kamishna Mkuu huyo amesema, miongoni mwa malalamiko ya wafanyabiashara wadogo katika soko la Kariakoo ni kutotoa Risiti za Kielektroniki (EFD).

Vilevile, kuingiza mizigo nchini kwa kuchangia kasha na hivyo mtu mmoja kulipia ushuru wa forodha.

“Tumetengeneza timu na wale wanaoigiza kwa kuchangia makasha, hii ni moja ya namna ya kutatua changamoto inayowakabili.

“Nyingine walitaka wajue makadirio ya kodi kabla hawajaagiza mzigo. Tumekubaliana tuwe na viwango vya makadirio kwa shehena mbalimbali."

CPA Mwenda amesema, bidhaa nane vikiwamo vitenge na nguo, zimeshawekewa makadirio ya ushuru wa forodha, hivyo kila mfanyabiashara anajua kiasi atakacholipa kabla ya kuagiza mzigo wake.

“TRA inataka kuona Kariakoo inakuwa soko lenye ushindani mkubwa kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Haipendezi kuita Soko la Kimataifa wakati watu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)hawaji. Tunaamini wakija wengi tutapata kodi zaidi na hili linawezekana."

Wakati huo huo, CPA Mwenda amesema, mamlaka hiyo inatengeneza mfumo utakaoziwezesha mamlaka zote za Serikali kusomana na kurahisisha kuwatambua wafanyabiashara wa ngazi zote kuanzia wadogo nchini.

“Tutajenga mifumo ya kodi za ndani na ya forodha. Kumekuwa na malalamiko mengi kwamba, mifumo haisomani na kutosomana kunapoteza kodi za Watanzania.

"Tutajenga Mfumo wa Forodha (TANCIS), ambao utazinduliwa Januari mwakani ili kuhakikisha kwamba, taarifa tunazozipata ni sahihi na zinatumika kutenda haki na kutoa uamuzi sahihi wa kodi.

“Tunaamini hii mifumo itatusaidia kuwajua wafanyabiashara ambao hawako kwenye taarifa za TRA. Tukiimarisha hii ninaamini tutaongeza tax base."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news