DAR-Tume ya TEHAMA nchini imesema kuwa, inashirikiana na Rais na Mkuu wa Chuo cha Turku, Prof.Vesa Pekka Taatila kutoka nchini Finland ili kuleta intaneti mpya inayotumia mikono zaidi kutengeneza mfano wa kitu halisi kwenye kompyuta na kuunganisha moja kwa moja kwenye matumizi ijulikanayo kama Metaverse.Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Dkt.Nkundwe Mwasaga wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkuu wa chuo hicho kuelezea umuhimu na ufanisi wa intaneti hiyo.
Amesema, kwa sasa intaneti inayotumika inasaidia kubadilisha na kupata taarifa katika kurasa, picha, video na kwamba teknolojia imekuwa zaidi ambapo kuna intaneti ya vitu ijulikanayo kwa jina la IOT ambayo inapelekea kuwa na intaneti ya Metaverse.
Amesema,mwaka jana walitembelea chuo hicho cha Turku na kuvutiwa na teknolojia hiyo ya intaneti mpya ya Metaverse ambayo amesema itasaidia upatikanaji wa kodi, takwimu, biashara na upatikanaji wa vitu bila kutumia gharama nyingine.
"Intaneti ya Metaverse inatengeneza kitu kama kilivyo, hivyo itaondoa tatizo la upatikanaji wa vifaa vya maabara,"amesema.
Kwa upande wake Mshauri Mkuu wa Uvumbuzi Kidigitali kutoka Tume hiyo, Dkt. George Mulamula amesema kuwa, kuja kwa mtaalam huyo kumetokana na dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka kuwepo na chuo cha tofauti na vyuo vingine vilivyopo hapa nchini.Amesema,kutokana na dhamira hiyo ya Rais tayari wataalamu wanafanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Teknolojia ya Kidigitali ambacho kinatarajiwa kujengwa mkoani Dodoma kwa lengo la kutatua changamoto za ajira, biashara na changamoto mbalimbali katika jamii.
Amesema, intaneti hiyo mpya kwa asilimia 75 inatumia zaidi mikono kutengeneza mfano wa kitu halisi kwenye kompyuta na kuunganisha moja kwa moja kwenye matumizi na asilimia 25 inatumia njia nyingine.
Amesema kuwa, teknolojia hiyo itatumika kwenye kilimo, uvuvi, madini, viwandani na kwenye maeneo mengine hususani katika sekta ya elimu.
Amesema kuwa, wameamua kushirikiana na mtaalamu huyo kutoka chuo hicho kwa kuwa ni wabobezi ambao watasaidia kuleta teknolojia hiyo hapa nchini ambapo Tume ya TEHAMA itajikita katika kutoa mafunzo jinsi ya kutumia mitaala hiyo kutengeneza ajira na kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Aidha,ametoa wito kwa jamii hususani vijana kuangalia ni jinsi gani wanaweza kutumia teknolojia katika kutatua changamoto ili kuleta mafanikio kwa jamii.