Tumia SGR

NA LWAGA MWAMBANDE

AGOSTI 1,2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi huduma za Usafiri wa Treni ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Sherehe za uzinduzi huo zilifanyika katika Stesheni Kuu ya Dar es Salaam, lengo likiwa ni kuboresha miundombinu na usafiri nchini Tanzania.

Aidha, tangu Mheshimiwa Rais Dkt.Samia afanye uzinduzi huo, tumeshuhudia maelfu ya Watanzania na wageni mbalimbali wakitumia treni hiyo ambayo licha ya kurahisisha safari kutoka Dar hadi Dodoma, pia imepunguza muda mwingi ambao wengi wetu tulikuwa tunautumia barabarani kwa magari.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande ni miongoni mwa Watanzania waliotumia usafiri wa treni hiyo na kufurahia safari salama na ya haraka kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam. Endelea;

1. Kama watoka Dodoma elekea Dasalamu,
Kwa haraka na salama, ufike Daresalamu,
Kuna njia tatu nzima, ambazo nazifahamu,
Tumia SGR.

2. Ya zamani losalia, na ambayo inadumu,
Barabara nakwambia, huko mpate salamu,
Muhimu mnabakia, kipya kimekwishatimu,
Tumia SGR.

3. Mabasi twayatumia, mengi yapeana zamu,
Saa zote yaingia, hata kutimia timu,
Chombo kipya shaingia, kukitumia kitamu,
Tumia SGR.

4. Magari madogo pia, yakimbizana kwa zamu,
Vema tunayatumia, muda wetu twajihimu,
Mkombozi kaingia, abeba wengi kwa zamu,
Tumia SGR.

5. Magari yanatumia, theluthi siku yatimu,
Dodoma ukianzia, Dasalamu ukatimu,
Mpya katupunguzia, muda tunavyofahamu,
Tumia SGR.

6. Garimoshi Tanzania, Kigoma tu Dasalamu,
Hilo bado labakia, nchini kwetu muhimu,
Huku tunafurahia, tunazidi kuhitimu,
Tumia SGR.

7. Ndege zinajirukia, zaenda zamu kwa zamu,
Watu zinawapakia, siyo wengi wanadamu,
Halafu kugharamia, zinawafaa wagumu,
Tumia SGR.

8. Treni mwendo sikia, kasi usoifahamu,
Toka pale yaanzia, Kilosa Moro yatimu,
Mbio ikifungulia, mara Dasalamu homu,
Tumia SGR.

9. Mwendokasi nakwambia, kila mtu mhitimu,
Siti anajikalia, kipupwe kikihudumu,
Mabehewa yavutia, kweli tumeshahitimu,
Tumia SGR.

10. Serikali Tanzania, hebu pokea salamu,
Reli mmetufanyia, kwa kweli mzidi dumu,
Kile kilichobakia, kutunza na kuhudumu,
Tumia SGR.

11. Magufuli lianzia, mradi kuuhudumu,
Kuondoka tulilia, mwingine kashika zamu,
Tulipo Mama Samia, azidi fanya matamu,
Tumia SGR.

12. Kule tulikoanzia, Moro hadi Dasalamu,
Dodoma tumefikia, mbio hadi Dasalamu,
Hamu kwetu yabakia, Mwisho wa Reli kutimu,
Tumia SGR.

13. Mwanza hakujasalia, ujenzi nako wadumu,
Nako tutakufikia, twaenda zamu kwa zamu,
Hili tunafurahia, tena latutia hamu,
Tumia SGR.

14. Heri tunaitakia, huduma hii idumu,
Nchi yetu Tanzania, mengi tuweze jikimu,
Uchumi weze fikia, pazuri penye karamu,
Tumia SGR.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news