Tuondoe vikwazo vya rufaa za matibabu Afrika Mashariki-Waziri Mkuu

DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watoa huduma za afya wa nchi wanachama wa kanda ya Afrika Mashariki kuondoa vikwazo vinavyozuia wagonjwa wanaotafuta matibabu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
"Hatua hii ni kwa manufaa ya wananchi wetu na kwa uchumi wa kikanda na ukuaji wa utalii tiba."

Ametoa wito huo leo Ijumaa Agosti 30, 2024 alipokuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 12 wa Shirikisho la Watoa Huduma za Afya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema,nchi wanachama ikiwemo Tanzania zimejitahidi kuwekeza katika sekta ya afya na kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya Kanda kwa matibabu.

"Kwa sasa ni wagonjwa wachache sana wanaosafiri nje ya nchi zetu kwa ajili ya matibabu, kwani karibu magonjwa yote makubwa sasa yanaweza kutibiwa ndani ya Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wa Sekta ya Afya kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa Serikali imetengeneza sera rafiki za uwekezaji hususan katika Sekta ya Afya kutokana na uhitaji wa huduma hizo nchini.

"Tunawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya afya, Sera nzuri tunazo, Sheria na kanuni nzuri tunazo, mahitaji ya uwekezaji kwenye sekta ya afya ni makubwa na tunataka tupate teknolojia mpya na huduma za kibingwa."
Kadhalika amewataka wadau wa afya wa kanda kujadili mbinu mbalimbali za kuimarisha mifumo ya afya na kuwa na mikakati ya pamoja ya kukabiliana na magonjwa.

"Tumieni jukwaa hili kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na magonjwa ya mlipuko, magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ambukiza pamoja na magonjwa mapya yanayotokana na mabadiliko ya hali ya tabia nchi."
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema, uwekezaji uliofanywa na serikali kuanzia ngazi ya chini umewezesha ugunduaji wa magonjwa yakiwa katika hatua za awali.
"Rufaa kwenda nje ya nchi zimepungua kwa kiasi kikubwa kipindi cha nyuma watu waliokuwa wanafika Ocean road walikuwa kwenye hatua za mwisho za ugonjwa, lakini kutokana na uwekezaji sasa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanakuja wakiwa na magonjwa katika hatua za awali."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news