NA ADELADIUS MAKWEGA
KANISA Katoliki limesema kuwa mara nyingi binadamu anaposafiri huwa anatilia maanani kutayarisha chakula cha njiani au hata kuchagua pahala sahihi pa kula.
Aidha,mara zote binadamu hukwepa kula au kubeba chakula kilichochacha na hivyo ndivyo inatakiwa kuwa hata katika kwenda mbinguni lazima kila mwanadamu kukitilia maanani chakula kisichoharibika ambacho ni Yesu Kristo mwenyewe.
Waumini wa Kanisa la Bikira Maria Malikia wa Wamisionari Parokia ya Malya Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza wakifuatilia mahubiri leo.
Hayo yamehubiriwa na Kadinali Luiz Antonie Tagle ambaye ni Kiranja na Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki anayoshugulikia Uinjilishaji wa Watu Ulimwenguni ndani ya mahubiri yake ya dominika ya 19 ya mwaka B wa Liturjia ya Kanisa kupitia runinga ya JesCom.
“Katika somo la pili la dominika hii Mtakatifu Paulo anasema, sisi kama wafuasi wa Yesu Kristo kila tunapokuwa safarini tukumbuke kuacha kubeba vyakula vilivyochacha.
"Je, vyakula vilivyochacha safarini ni vipi? Hasira, chuki kashfa, maneno mabaya kwa wengine.
"Baadhi ya vyakula vinavyofaa safarini ni ukarimu, wema na upendo.”
Akipigilia msumari wa mahubiri ya dominika hii Padri Samson Masanja wa Kanisa la Bikira Maria Malikia wa Wamisionari Parokia ya Malya Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza alisema kuwa;
“Fundisho la Kristo katika domonika ya leo ni juu ya uwepo wake na juu ya safari yake ya kumkomboa mwanadamu, kwa sadaka yake Kristo anafanywa kuwa chakula cha uzima na anabakia kwetu kama chakula cha uzima na hapa tunaunganika na mweenyenzi Mungu.”
Akiendelea kuhubiri katika dominika hii Kadinali Tagle alisema kuwa
“Dominka ya 19 ni wajibu wa kila mmoja kufungua kapu lake safarini na ajitafakari amejitwika chakula gani yeye kama mfuasi wa Kristo?”
Naye Padri Masanja akihitimisha mahubiri yake alisema kuwa kila Mkristo anapaswa kufuata mafundisho ya Yesu Kristo na kuzishika amri za Mungu.
Kwa hakika hapa Malya na viunga vyake kwa juma zima na hadi misa hiyo ya kwanza inamalizika majira ya saa mbii ya asubuhi, hali ya hewa ni ya baridi kidogo nyakati za asubuhi na jua la kadili nyakati za mchana