Ufanisi wa NHC wamgusa Waziri Ndejembi

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuendelea kuonesha umahiri mkubwa katika ujenzi wa nyumba bora na za kisasa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah akitoa wasilisho la utendaji wa shirika hilo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi makao makuu ya shirika hilo leo Agosti 9,2024 jijini Dar es Salaam.

Ameyabainisha hayo leo Agosti 9,2024 baada ya kutembelea rasmi makao makuu ya NHC yaliyopo Kambarage House jijini Dar es Salaam.
Lengo la ziara ya Mheshimiwa Waziri Ndejembi ni kujitambulisha kwa watumishi wa shirika hilo na kufahamu mikakati waliyonayo katika kuhakikisha Watanzania wanakuwa na makazi bora nchini.

Mheshimiwa Ndejembi aliteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo kuchukua nafasi ya Mheshimiwa Jerry Silaa, na kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam Julai 26, 2024, kufuatia uteuzi, utenguzi na uhamisho uliofanywa Julai 21, 2024 na Rais Dkt. Samia.

"Shirika linaenda vizuri,mnaingiza faida vizuri chini ya uongozi mahiri kabisa wa Mkurugenzi Mkuu hapa inaonesha umahiri wake na ukuaji unaonekana.
"Lakini, katika ukuaji, tusisahau malengo mazima ya Shirika la Nyumba la Taifa. Uanzishwaji wake wa mwaka 1962 ulikuwa kwa malengo ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na makazi bora.

"Na Watanzania waliowengi ni wa kipato cha chini,kwa hiyo ni muhimu kadri tunavyokuwa tusiwasahau,tusiwaache nyuma.

"Tuhakikishe kwamba tunakuja na mipango mizuri ya kuhakikisha Mtanzania yule anayejenga nyumba yake taratibu kwa fedha ambayo anaipata aidha kwenye kazi, akiba yake kutokana na kazi au ni mjasiriamali anajenga kutokana na akiba anazozipata kwenye kazi zake za kila siku.
"Basi sisi tumrahisishie ile ndoto yake ya kuwa mmiliki wa nyumba kwa maana tutengeneze nyumba ambazo zitakuwa ni nafuu kwa wote.

"Tuhakikishe nyumba zenyewe pia ziwe zenye viwango bora,na zipo kwenye maeneo ambayo ni rahisi kwa mtu kufika.

"Maana yake nikisema nafuu, simaanishi uende kuiweka kilomita 100 kwa mtu ambapo anafanya shughuli zake za kila siku.

"Kwa hiyo, tusisahau wala tusiache malengo yaliyoanzisha shirika la nyumba na maono ya Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhakikisha Watanzania wanapata nyumba.
"Lingine ni hili la kuhakikisha miradi yetu inakuwa na value for money. Changomoto tunawaacha wengi kwenye ununuzi wa nyumba hizi kwa sababu, miradi hii mpaka inakamilika uniti moja mtu anapiga hesabu nikanunue nyumba ya milioni kadhaa ambayo ni shared facilities, ninaweza nikachukua hii nyumba nikaenda Mapinga au kwingineko nikajenga nyumba yangu na ikakamilika.

"Sasa over price inatokana na nini? Umeweka vizuri sana (Mkurugenzi Mkuu wa NHC) kwamba ni ile kutokuwa na efficiency katika miradi.

"Sasa, mimi ninawaomba sana mkaongeze efficiency katika miradi, efficiency hiyo kivipi? Kuhakikisha kwamba hatua mlizochukua za kuweka biometrics, kuhakikisha kwamba yule aliyekuja kibarua kweli amefika.
"Kuhakikisha kwamba hakuna wizi wa materials kwenye site, lakini kuhakikisha pia tunapokwenda kununua ardhi sehemu tunapata ile bei halisi bila kutanguliwa na mtu mbele.

"Sasa, wewe (NHC) lazima uingize kwenye bei ya zile uniti, kwa hiyo ili ningependa kuomba tuhakikishe miradi yetu inakuwa na value for money, ningetamani sana kuona hilo,"amesisitiza kwa kina Mheshimiwa Ndejembi.

Pia, amewapongeza kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati nchini. "Kupitia Samia Housing Scheme mna malengo ya kujenga nyumba zaidi ya 5,000 ambapo awamu ya kwanza ndiyo inaenda kukamilika, ni jambo jema sana."
Pia, ameshauri mradi kama huo uelekezwe zaidi katika maeneo ambayo kuna wanunuzi wengi wa nyumba ambao hawajafikiwa na miradi hiyo.

Vile vile amesema, wakati umefika kwa NHC kuweka mipango ambayo itamsaidia mtu mwenye kipato cha chini kumiliki nyumba za shirika kupitia utaratibu rafiki hata ndani ya miaka 10.

“Mnapaswa kuanzisha utaratibu wa kulipa kiasi fulani cha asilimia ya gharama ya nyumba na kuruhusu mteja huyo kuanza kuishi huku akiwa analipa kiasi kidogo cha fedha kila mwezi mpaka atakapomaliza deni lake” amesema.

NHC

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah akitoa wasilisho la utendaji wa Shirika kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa mwaka 1962 kwa Sheria Na.45 kwa lengo la kuwapatia wananchi makazi bora.
"Na bahati nzuri lilikuwa ni shirika la kwanza kuanzishwa na Mwalimu Nyerere mwaka mmoja tu baada ya Uhuru wa nchi yetu."

Amesema, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitoa kipaumbele cha kwanza kuanzishwa shirika la nyumba kutokana na umuhimu wake kwa wananchi.

"Staha ya binadamu mbali na mavazi pia makazi ni muhimu, kwa hiyo akaona wakati huo nchi yetu,kama Dar es Salaam ilikuwa kwenye zones.

"Ukienda Oysterbay wanakaa Wazungu, ukienda Upanga wanakaa tabaka lingine na Waswahili wenzetu wanakaa kuanzia Magomeni, Magomeni Mapipa, makazi yao hayakuwa mazuri Makuti na kwingineko.
"Kwa hiyo (Mwalimu Nyerere) akaona kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora.Kwa hiyo, ndiyo maana likawa shirika la kwanza kabisa kuanzishwa hapa nchini."

Amesema, wakati shirika hilo linaanzishwa Serikali ilikuwa ikitoa ruzuku ya asilimia 47 huku nchi rafiki ya Ujerumani Magharibi ikiwa inatoa usaidizi wa asilimia 40.

"Ukiunganisha pamoja na mikopo ambayo tulikuwa tunapata wakati ule ilikuja ikaanzishwa Benki ya Nyumba ambayo nayo ilikuwa inatupatia mikopo."
Mkurugenzi Mkuu huyo ameeleza kuwa, kupitia ruzuku ambayo Serikali ilikuwa inatoa ya asilimia 47 ililifanya shirika liweze kujiendesha kibiashara kwa kuanzisha nyumba, kupangisha na kuziuza.

Amesema, kutokana na jitihada hizo shirika hilo lilifanikiwa kutekeleza miradi mingi mpaka mwaka 1979 hadi 1980 ambapo zaidi ya nyumba 14,000 zilijengwa na shirika hilo.

"Lakini, kama mnakumbuka historia vizuri miaka 1978-79 nchi yetu iliingia katika vita ya Uganda ambapo rasilimali nyingi za Serikali zilielekezwa kwenye vita na uwezo wa Serikali kutoa ruzuku kwa shirika ukawa umepungua sana.
"Kwa hiyo, miradi ikawa haiendi tena likawa sasa linategemea zaidi kujiendesha kwa pesa ambazo zinatokana na mapato yake yenyewe."

Pia, amesema kwa upande wa nchi rafiki nako mambo yalibadilika huku benki nayo ikawa taabani hadi kufikia hatua ya kufilisika kabisa.

"Kwa hiyo, Serikali ikaona umuhimu sasa ulipofika mwaka 1990 ikaona hakuna sababu ya kuliacha shirika likaendelalea na hali hiyo, kwa hiyo shirika likaundwa upya."

Amesema,NHC lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 45 ya mwaka 1962 kabla ya kuunganiswa na iliyokuwa Msajili wa Majumba kwa Sheria namba 2 ya mwaka 1990, ambayo ilirekebishwa mwaka 2005 ili kulifanya shirika lijiendeshe lenyewe kibiashara.

"Kwa hiyo shirika likaundwa upya kwa Sheria Na.2 ya mwaka 1990 na wakati huo kwa sababu uwezo wa shirika ulikuwa mdogo wakasema waliongezee nguvu.
"Kwa kuliunganisha na shirika lingine ambalo lilikuwa linaitwa Msajili wa Majumba (Registers of Building) zamani ulikuwa ukipita miji yetu yote majengo mengi utaona yameandikwa Msajili wa Majumba.

"Kwa hiyo baada ya kuunganishwa Shirika la Nyumba likawa limebaki, Msajili wa Majumba ikawa imekufa."

Amesema, licha ya jitihada zote hizo za Serikali ambazo ilikuwa inafanya bado ufanisi wa shirika haukuwa mzuri.

"Mwaka 2005 wakati huo ameingia Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ikaonekana moja ya sababu ambayo ilikuwa inafanya shirika lisifanye vizuri ilikuwa ni Sheria ya Ukomo wa Kodi ya Pango ikapelekwa proposal kuwa moja ya sheria ambayo inafanya Shirika la Taifa la Nyumba lisifanye vizuri ilikuwa ni Sheria ya Ukomo wa Kodi ya Pango ya mwaka 1984."

Amesema,sheria hiyo ilifanyiwa maboresho mwaka 2005 na maboresho mengine pia kufanyika ili kuwezesha shirika kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kibiashara zaidi.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, miongoni mwa majukumu ya shirika hilo ni kujenga nyumba za makazi na majengo mengine kwa ajili ya kupangisha na kuuza.

"Kwa hiyo tunajenga na kuuza kwa sababu ni sehemu ya biashara na umuhimu wake ni kuwa tusiwafanye Watanzania wabaki kuwa wapangaji, tuweze kuwawezesha vile vile waweze kuwa wamiliki wa nyumba."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news