Uongezaji thamani madini ni kipaumbele cha Serikali-Dkt.Kiruswa

DAR-Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Kiruswa, amesema Uongezaji Thamani Madini ni moja ya vipaumbele vikuu vya Wizara, ambapo msukumo mkubwa umewekwa kupitia Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na kuongeza kwamba, Sheria ya Madini inaelekeza kuhakikisha kuwa madini yanaongezwa thamani ndani ya nchi ili kuongeza manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo Agosti 23, 2024, wakati akifunga mafunzo ya Siku tatu ya uongezaji thamani madini ya vito kwa nadharia na vitendo kupitia mradi wa Pamoja Initiative yaliyoandaliwa na Chama cha Tanzania Women in Mining and Mineral Industry (TWIMMI).
Mafunzo hayo yamefanyika katika Kituo cha Madini na Jiosayansi African Minerals and Geosciences Centre (AMGC) jijini Dar es Salaam huku mafunzo kwa vitendo yakitarajiwa kufanyika kwa kutembelea moja ya migodi mkoani Morogoro.

‘’Hivi sasa maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha leseni kubwa za uchimbaji Madini Mkakati zinazotolewa zinazingatia sharti la madini hayo kuongezewa thamani ndani ya nchi,’’ amesisitiza Dkt. Kiruswa.
Kufuatia msukumo huo wa Serikali wa kuongeza thamani ndani ya nchi, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ametoa wito kwa Watanzania hususan vijana na wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali za uongezaji thamani kupitia madini ya vito ambayo Tanzania imebarikiwa kuwa nayo aina mbalimbali.

“Mnyororo wa uongezaji thamani madini unafaidisha watu wengi ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na kutoa ajira, kukuza teknolojia na kuongeza mapato kwa Serikali.
"Mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunakuwa na wataalamu wabobezi ndani ya nchi wanaoendana na teknolojia za kisasa za uongezaji thamani madini na pia kuendelea kufanya mabadiliko ya Sheria ili kuzuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi,” amesema Dkt. Kiruswa.

Dkt. Kiruswa ameeleza kuhusu jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha shughuli za uongezaji thamani madini zinafanyika nchini zikihusisha madini mengine mbali na vito na kutoa mfano wa viwanda vya kusafisha dhahabu vilivyojengwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo matarajio ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha usafishaji madini ya metali cha Tembo Nickel Refining Limited kitakachojengwa Wilayani Kahama.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameutaka uongozi wa Kituo cha AMGC kuweka ushirikiano wa karibu na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili kuhakikisha vinazalisha wataalam waliobobea katika shughuli za uongezaji thamani madini ya vito pamoja na kuzalisha bidhaa zenye viwango vya juu ikiwemo matumizi ya vifaa vya kisasa.

Ametumia fursa hiyo kuipongeza TWiMMI kwa kuandaa mafunzo hayo yaliyowashirikisha vijana wapatao 40 kutoka vyama mbalimbali vya wachimbaji wadogo wakiwemo wanawake, vijana, wahitimu wa vyuo vikuu na TGC, waongezaji thamani madini, watoa huduma wafanyabiashara wa madini na washiriki wengine vijana kutoka nchi za Kenya, Rwanda na Afrika Kusini.
Aidha, Naibu Waziri pia ameelezea kuhusu Programu mpya ya "Mining for Brighter Tomorrow" (MBT) inayolenga kuwainua wachimbaji wanawake na vijana kupitia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini na kuwataka vijana kuunda vikundi vya uchimbaji ili waweze kunufaika na programu hiyo, ambayo itahusisha kuwapatia leseni na vitendea kazi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amegawa vifaa maalum 30 vya utambuzi wa madini ya vito kwa washiriki wa mafunzo hayo na kusisitiza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia katika kuendeleza shughuli zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha AMGC Ibrahimu Shaddad amewataka vijana nchini kukitumia kituo hicho kijifunza masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za uongezaji thamani madini na kusema ‘’ Tutaendelea kuweka nguvu kuhakikisha kituo hiki kinakuwa na manufaa kwa nchi wanachama na watanzania.’’Naye, Mwenyekiti wa TWIMMI,Palina Ninje ameiomba Wizara kuwapatia eneo la pamoja la kuchimba kuchimba kupitia umoja wao ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji pamoja na kuiomba Wizara kuzungumza na taasisi za fedha ili zitoe mikopo nafuu kwa vijana na wanawake waliopo katika Sekta ya Madini.
"Pamoja na hayo Mhe. Naibu Waziri tunaipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa semina mbalimbali kwa vijana, wanawake pamoja na kutoa vifaa vinavyowasaidia katika shughuli zao,’’ amesema Palina.

Pia, ameupongeza uongozi wa kituo hicho kwa kukubali kutoa nafasi kwa vijana kujifunza katika kituo hicho ambacho kimekuwa na uzoefu katika shughuli hizo kwa miaka mingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news