Uongozi wa TCB wateta na Spika Dkt.Tulia,mema yanakuja kwa wajasiriamali

DODOMA-Katika jitihada za kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za kifedha na mihimili ya Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Bw. Adam Mihayo amemtembelea na kuzungumza na Spika wa Bunge la Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson.
Bw. Mihayo ameambatana na Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati wa benki hiyo, Bi. Lilian Mtali, katika ziara hiyo ambayo inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya Benki ya TCB na Bunge la Tanzania katika kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati nchini.

Mazungumzo na kiongozi huyo wa Bunge linaloundwa na wabunge 393 kutoka majimbo 239 yamejikita katika masuala nyeti yanayohusu majimbo mbalimbali katika jitihada za kuendelea kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati.
Wakitambua mchango mkubwa wa kundi hili katika ukuaji uchumi na uzalishaji wa ajira mpya, mazungumzo yao yamejikita katika kuanzisha mpango wa ruzuku, mikopo ya riba nafuu, na misamaha ya kodi kwa wajasiriamali.

Miradi hii itasaidia kukuza na kuchochea mazingira ya biashara kwa wajasiriamali pamoja na biashara zao.

“Lengo letu sio kutoa jibu moja kwa nchi nzima.Huwezi kuwa na suluhisho moja kwa watu wote, ndiyo maana ni muhimu kuwasikiliza wadau wengi kadri iwezekanavyo.
"Njia hii itatusaidia kutoa majibu yatakayokidhi mahitaji ya wajasiriamali kulingana maeneo wanayoishi hata wale walioko vijijini,” amesema Bw. Mihayo.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Spika Dkt. Tulia Ackson amebainisha umuhimu wa ushirikiano huo na kusisitiza wajibu wa Bunge katika kutunga sera zinazowezesha maendeleo ya wajasiriamali na kuhakikisha kwamba biashara zao zinapata rasilimali zinazohitajika ili kukua.

“Maendeleo ya wajasiriamali ni muhimu kwa ukuaji uchumi wa taifa letu, kupitia ushirikiano huu na Benki ya TCB, tunaweza kutengeneza mazingira yatakayowezesha ukuaji wa biashara,“ amesema.

Kikao hicho kimehitimishwa kwa azimio la ushirikiano wa pamoja na kuendelea kubuni nyanja mbalimbali za ushirikiano lengo likiwa kuinua sekta ya wajasiriamali nchini.
Ushirikiano huu unategemewa kufungua miradi mbalimbali itakayosaidia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news