Ushiriki wa BoT maonesho ya Nanenane unawezesha wananchi kuifahamu benki-Gavana Tutuba
DODOMA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, ametembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma.
Gavana Tutuba alieleza kuwa ushiriki wa BoT katika maonesho hayo unawawezesha wananchi kupata uelewa sahihi wa shughuli za Benki Kuu na jinsi inavyosaidia katika ustawi wa uchumi wa nchi.
Aidha, alisema kuwa Maonesho ya Nanenane yanatoa fursa kwa BoT kuwafikia wananchi wengi moja kwa moja, na pia kujua changamoto na maoni ya wananchi kuhusu huduma za fedha nchini, namna yakuziboresha na kuhakikisha kuwa zinawafikia wananchi kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.
Gavana Tutuba alisisitiza kuwa ni muhimu kwa kila mwananchi kuwa na uelewa wa masuala ya fedha ili aweze kufanya maamuzi sahihi yanayoweza kuboresha hali yake ya maisha na uchumi wa taifa kwa ujumla.