DAR-Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga amesema, katika kuhakikisha tatizo la dawa za kulevya linatokomea nchini Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar wataendeleza ushirikiano katika mapambano hayo.Mhe. Ummy ameyasema hayo Agosti 20, 2024 jijini Dar Es Salaam wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi la Kusimamia Ofisi ya Viongozi Wakuu Zanzibar na ujumbe kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA).
Lengo ni kutembelea na kujifunza masuala mbalimbali ya namna ambavyo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inavyofanya kazi.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo akizungumza katika kikao hicho.
“Nikuhakikishie Mwenyekiti tutaendelea kudumisha mashirikiano yetu kati ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Wizara zote kuhakikisha kwamba tunaboresha mahusiano yetu baina yetu kwa ajii ya kufanya kazi hii nzuri ambayo baadae yana malipo mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sababu kazi hii siyo yetu peke yetu lakini pia kwa nafasi zetu tuendelee kuwajibika na kufanya kazi zetu,” alisema Naibu Waziri Ummy.
Sambamba na hayo Mhe. Ummy amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi kwa kuendelea kuziwezesha Mamlaka zote mbili katika mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya nchini.
“Niwapongeze viongozi wetu ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi kwa Juhudi za kuhakikisha Mamlaka zote zinapata fedha pamoja na Rasilimali zingine kwa ajili ya kuimarisha mapambano haya ya Dawa za Kulevya,” aliongeza Naibu Waziri Ummy.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi la Kusimamia Ofisi ya Viongozi Wakuu Zanzibar Mhe. Machano Othman Said amesema, kutokana na mabadiliko ya maendeleo yaliyopo Bara kamati iliamua kuja kujifunza na kupata uzoefu wa namna Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) inavyofanya kazi kwa ajili ya kutokomeza suala la Dawa za Kulevya.
“Mheshimiwa Naibu Waziri sisi tunakuja sana Bara na tumeona mabadiliko ya maendeleo ambayo yanayofanywa na Dkt. Samia lakini na ninyi mnakuja Zanzibar na mnaona mabadiliko makubwa ya maendeleo yanayofanywa chini ya Dkt. Hussein Mwinyi sasa leo kamati yangu imeamua ije kuangalia wenzetu wanafanya kazi vipi chini ya mamlaka.”
“Sisi Zanzibar Kanali Nassor na wenzake wanajitahidi sana kwa sababu miaka minne au mitano nyuma suala la Dawa za Kulevya Zanzibar lilikuwa halipewi uzito mkubwa tulikuwa tunakitu kinaitwa tume lakini kwa sasa ninafurahi kuwa ripoti tunazopata kupitia Kanali Nassor na timu yake kuwa kuna mahusiano mazuri ya kazi na hicho ndicho kilichotufanya tuje kujifunza namna mamlaka inavyofanya kazi,” alibainisha Mhe. Machano.
Kamati ya Baraza la Wawakilishi linalosimamia Ofisi ya Viongozi Wakuu Zanzibar imefanya ziara hiyo ya kikazi ya kutembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa namna mamlaka hiyo inavyofanya kazi zake.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
Ofisi ya Waziri Mkuu