Vijana 3,000 kushiriki kongamano Dodoma

NA DIRAMAKINI

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema Vijana 3000 kutoka maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kushiriki kwenye Kongamano la vijana Agosti 10 hadi 11, 2024 jijini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma.

Mhe. Katambi amebainisha hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Vijana kimataifa ambayo yamebeba kauli mbiu isemayo “Vijana na matumizi ya fursa za kidijitali kwa maendeleo Endelevu”.

Amesema kuwa, kupitia Kongamano hilo, vijana watapata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, na kujadili fursa za vijana na matumizi ya kidijitali, vijana na afya na uchumi.

"Lengo kuu la kuadhimisha Siku ya Vijana ya Kimataifa ni kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa na jamii kwa ujumla kupata fursa ya pamoja ya kusherehekea na kutambua nafasi na mchango wa vijana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwenye nchi zao, tanzania tukiwemo,"alisema Katambi.

Aidha, Mhe. Katambi amesema kuwa vijana ndio nguvu kazi, wabunifu na chachu ya mabadiliko katika jamii yoyote ile. Vijana ndiyo warithi wa historia katika Mataifa yao, hivyo serikali itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika kukuza maendeleo nchini.

Vile vile, amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka 2023 hadi 2024 imetoa ajira 607, 475 ambapo zilizotolewa na serikali ni 43,469, ajira kutokana na Miradi ya serikali 204, 959 na Ajira katika sekta binafsi 359,052.

Kwa upande mwengine, Mhe. Katambi amesema serikali itaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia Wizara za kisekta ili kundi hilo kujikwamua kiuchumi. Sambamba na hayo ametoa wito kwa vijana kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.

Agosti 12, 2024, itakuwa ni siku ya kilele cha Siku ya Vijana Kimataifa, ambapo vijana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana watashiriki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news