MARA-Waziri wa Madini,Mhe.Anthony Mavunde ametaka fedha zinazotolewa kama sehemu ya gawio la mrabaha kutoka katika mgodi zitumike katika miradi iliyoibuliwa na wananchi katika sehemu husika kwa ajili ya kuendeleza mipango ya maendeleo kwa wananchi.


Akielezea kuhusu ushirikishwaji wa vijana, wanawake na wazee katika sekta ya madini eneo la Nyamongo, Waziri Mavunde ameigiza Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Tarime kushirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Mara kutenga maeneo maalum yatakayofanyiwa utafiti na kugawiwa kwa makundi hayo kwa ajili kufanya uchimbaji wenye tija.
Akifafanua kuhusu mpango wa utekelezaji wa Maudhui ya Ndani (Local Content), Waziri Mavunde amesema, Wizara ya Madini itashirikiana na Wizara ya Kilimo kwenye mradi wa uchimbaji visima vya maji kuchimba visima katika eneo la Nyamongo ili kuongeza fursa ya upatikanaji wa maji kwa kilimo cha mbogamboga kama walivyoanza.
Awali, akiwasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya utoaji wa gawio la mrabaha wa asilimia moja kwa vijiji vitano Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara,Apolinary Lyambiko amesema, kampuni ya Twiga katika Robo ya Pili ya mwaka 2024 imetoa mrabaha wa zaidi ya shilingi bilioni 1.1 katika vijiji vitano ikifanya jumla ya shilingi bilioni 2.2 kutolewa kwa vipindi vya robo ya kwanza na ya pili ya mwaka.
Lyambiko amevitaja vijiji hivyo nufaika kuwa ni pamoja na Kerende, Kewanja, Nyamwaga, Nyangoto na Genkuru.
North Mara Gold Mine Limited imeendelea kutoa gawio la mrabaha kwa vijiji vitano ambavyo vilikuwa vikimiliki maeneo yenye leseni za uchimbaji (PML) wakati mgodi unaanzishwa na Kampuni ya Afrika Mashariki Gold Mines Limited (Sasa North Mara Gold Mine Limited) mnamo Aprili 27, 1996.

Lyambiko ameongeza kuwa, kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 kiasi cha bilioni 69 kimelipwa kwa Serikali ikiwa ni malipo mbalimbali yanayotokana na mgodi.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,Mhe.Masache Kasaka ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya madini hususani kwenye uwazi katika utoaji wa mirabaha.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Tarime Vijijini,Remi Mkapa ameishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wa Nyamongo kwa kuweka mpango wa wazi katika utoaji wa mrabaha ambapo kupitia fedha hizo jamii itaibua miradi ya kijamii na kutatua changamoto zilizopo.