Wa kula ndiye aliwa!

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA Biblia Takatifu katika kitabu cha 2Wakorintho 4:8-9 neno la Mungu linasema, "Pande zote twadhikika, bali hatukati tamaa. Twaudhiwa, bali hatuachwi, twatupwa chini bali hatuangamizwi".
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, licha ya mshangao wa Dunia, lakini bado kuna tumaini mbele yako, usikate tamaa piga hatua songa mbele. Endelea;

1. Kati ya anayetunga, na yule anatungiwa,
Nani vema kujipanga, ili aweze changiwa,
Aweze kuungaunga, pale ametindikiwa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

2. Nyimbo zake ametunga, vema zimesanifiwa,
Kwa pesa akajipanga, ziweze kurekodiwa,
Na huo wake uchanga, hata hakusaidiwa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

3. Idadi ameijenga, wasikiza asifiwa,
Sasa pale ajipanga, aweze kutangaziwa,
Wajuba wanamgonga, nyimbo hawezi pigiwa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

4. Kama njia imenyoka, hana wa kumuelewa,
Zingine zinasikika, wenzake wanasifiwa,
Yeye kajaa mashaka, jinsi anavyobaniwa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

5. Apita kuulizia, wale wametanguliwa,
Ngazi vipi wapandia, jamii yawaelewa,
Yao akizingatia, zaidi afilisiwa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

6. Kumbe kuna vifurushi, kama simu sawasawa,
Kuzipiga hawakeshi, endapo ukiishiwa,
Wala hawakuvumishi, watu waweze elewa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

7. Ndiyo tofauti yetu, watu tusioelewa,
Wakati huo wenzetu, kazi wanafanikiwa,
Huku hatupati kitu, upepo tunatolewa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

8. Vina vinaandaliwa, na watu wanaimbiwa,
Maneno washangiliwa, jina kubwa unapewa,
Mafao unaishiwa, ni kama unaonewa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

9. Mwisho watu wanachoka, jinsi walivyotumiwa,
Hamsini wanashika, vipaji vinafukiwa,
Makopo si takataka, mahali yanatakiwa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

10. Kama umetangulia, pengine utajiliwa,
Kama unasubiria, tama itashikiliwa,
Kweli watakusifia, na hata kushangiliwa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

11. Wanakula wanogewa, kitanzi unafungiwa,
Madini yapakuliwa, kwingine yaivishiwa,
Kile wewe waletewa, unaweza kupaliwa,
Dunia ni mshangao, wa kula ndiye aliwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news