Waandishi wa Sheria na Mawakili wa Serikali wakumbushwa wajibu wao wakati wa kuandaa sheria ndogo

DODOMA-Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Uandishi wa Sheria imeendesha mafunzo maalumu kwa Waandishi wa Sheria na Mawakili wa Serikali huku lengo kuu likiwa ni kuwakumbusha juu ya wajibu na masuala ya kuzingatia wakati wa kuandaa na kurekebisha Sheria ndogo na Kanuni mbalimbali.
Mafunzo hayo yamefanyika Agosti 12, 2024 katika ukumbi wa Msekwa Bungeni jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole, amesema mafunzo hayo ni mahususi kwa Waandishi wa Sheria na Mawakili yakilenga kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali zinazoibuliwa na Kamati ya Bunge ya Sheria ndogo, na kuongeza ufanisi wakati wa uandaaji na uandishi wa Sheria ndogo na Kanuni.

“Mafunzo ya leo ni maalumu katika kupitishana kwenye hizo changamoto zinazoibuliwa na Kamati ya Kudumu ya Sheria ndogo ya Bunge, pia ni sehemu ya kujifunza ili tusiendelee kurudia tena hizo changamoto, hivyo yalikuwa mafunzo muhimu sana kwa waandishi wa sheria na warekebu wote kuhudhuria."Aidha,Mwandishi Mkuu wa Sheria ameongelea juu ya Miongozo iliyotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo amesema hivi karibuni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetoa mwongozo kuhusu utaratibu wa uwasilishaji wa marekebisho ya Sheria, Kanuni pamoja na utengenezaji wa Kanuni mpya, na mwongozo mwingine ni kuhusiana na utaratibu wa kushughulikia hoja zinazoibuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo.
Mwandishi Mkuu wa Sheria ameendelea kusema kuwa lengo kubwa la kutoa Miongozo hiyo ni kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikijtokeza kwenye sheria na kanuni mbalimbali ambazo zinakuja kufanyiwa marekebisho, pia ameelezea kuwa malalamiko kwenye baadhi ya Kanuni kutokidhi malengo yaliyokusudiwa kumepelekea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa maelekezo mahususi katika kutatua changamoto hiyo.

“Baadhi ya Kanuni zimekuwa zikilalamikiwa kutokidhi malengo yaliyokusudiwa kwasababu ya kutokuwa na maelekezo toshelevu kutoka kwenye Wizara husika, hali hiyo imepelekea Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa maelekezo ya kuhakikisha kwamba maelekezo yote ya kutunga sheria na kanuni au marekebisho ya Sheria na Kanuni yanakuja yakiwa toshelevu ili kuwawezesha waandishi wa sheria kutengeneza au kurekebisha kanuni au sheria ambayo itakidhi yaliyokusudiwa.”Akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo kwa Waandishi wa Sheria na Mawakili wa Serikali, Mwandishi Mkuu wa Sheria Msaidizi Bw. Nicodemus Chuwa amesema mada kuu zilikuwa ni majukumu ya Mwandishi wa Sheria wakati wa kuandaa Sheria ndogo, na kupitia nyaraka mbili zilizotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kwenda kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kuhusu namna ya kuwasilisha mapendekezo ya kutunga au kurekebisha Kanuni, na namna ya kujibu hoja kutoka kwenye Kamati ya Sheria ya ndogo.

Katika hatua nyingine Mwandishi Mkuu wa Sheria Msaidizi, amesema baada ya mafunzo hayo ni mategemeo yake kuwa barua za kuleta mapendekezo ya maboresho au kutungwa kwa Kanuni zitakuwa zinajieleza kwa kina ili kumuwezesha Mwandishi wa Sheria kupata taarifa zote muhimu, kwakuwa Waandishi wa Sheria wanahusika kwenye vikao vya Wizara, Idara au Taasisi wakati wa wa maboresho au utungwaji wa kanuni.
Kwa upande wake Wakili wa Serikali Stephano Mbutu, kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo amepongeza Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kuaandaa mafunzo hayo kwani yanawasaidia Mawakili na Waandishi wa Sheria kuongeza ujuzi kunakopelekea kuwa ufanisi kwenye kazi zao.

“Nimpongeze mtoa mada pamoja na wote waliochangia maoni mbalimbali hakika mafunzo yatasaidia kutoongezea ujuzi na ufanisi kwenye masuala mbalimbali ya uandishi wa Sheria.”

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utaratibu wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa Waandishi wa Sheria, Warekebu na Mawakili wa Serikali kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kutimiza majukumu yao kwa ubora na weledi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news