Wadau wa maendeleo wahimizwa kushiriki kwenye usimamizi wa maafa

DAR-Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amesema nchi imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa.
Sambamba na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu na uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira.
Akizungumza Agosti 19, 2024 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Watoa Huduma za Kibinaadamu nchini, Brigedia Ndagala amebainisha kuwa, suala la kuzuia na kukabiliana na majanga ni mtambuka na linahitaji nguvu za pamoja katika kulishughulikiwa hivyo, leo suala hili linajidhihirisha wazi kwa kuona washiriki waliopo hapa kutoka katika Idara, taasisi za serikali na taasisi zisizo za kiserikali hawa wote ni wadau muhimu katika kushughulikia usimamizi wa maafa hapa nchini.
"Kipekee ninapenda kuwashukuru washirika na wadau wa maendeleo zikiwemo nchi rafiki, Umoja wa Mataifa, taasisi na mashirika ya kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, ambayo yameendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuiletea nchi yetu maendeleo, mchango wao umekuwa wa muhimu katika kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo kulingana na mipango tuliyojiwekea katika kukabiliana na suala hili la maafa," alisema Brigedia Hosea Ndagala.

Kwa upande wake Mtaalam wa Maafa na Uratibu wa Misaada ya Kibinaadamu Bw. Ruger Kahwa amesema, Tanzania inatambua na kuenzi siku hiyo muhimu inayokumbusha utu na kutuleta pamoja kuthamini ubinadamu, kutetetea maisha ya waathirika wa maafa, na utoaji wa misaada ya kibinadamu yenye hadhi na inayojali upatikaji wa mahitaji yanayojali utu.
"Sheria Mpya ya Usimamizi wa Maafa ya 2022 na Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022 – 2027) unatambua nafasi ya watoa misaada ya kibinadamu pia Sera ya Maafa inatoa wito wa kujumuishwa kwa wahusika na watoa misaada ya kibinadamu wa ndani na nje katika maandalizi na mifumo ya kukabiliana na maafa.

“Mbali na hayo, Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022 – 2027) unaangazia umuhimu wa kuongeza uelewa wa umma na elimu kuhusu hatari za maafa, jambo ambalo linaendana na malengo ya siku ya kimataifa ya watoa misaada ya kibinadamu, ya kuheshimu juhudi za misaada kibinadamu duniani kote na kuhamasisha msaada kwa watu walioathirika na maafa," aliongeza Bw. Ruger Kahwa.
Maadhimisho ya Siku ya Watoa Huduma za Kibinaadamu yalifanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwaka 2023 jijini Dar es salaam kwa kuandaliwa na Idara ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la RAPID -Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news