NA GODFREY NNKO
MVUA chache zinazotarajiwa katika msimu wa Vuli mwezi Oktoba hadi Desemba,2024 zinaweza kuathiri upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo na chakula kwa ajili ya samaki.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a ameyasema hayo leo Agosti 22,2024 jijini Dar es Salaam.
Ni mbele ya wanahabari wakati akiwasilisha taarifa kuelekea mvua za Vuli mwezi Oktoba hadi Desemba,2024.
Utabiri huo ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikihusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba.
Pia,Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Kaskazini mwa Kigoma.
"Hali hii inatarajiwa kuathiri uzalishaji wa mifugo, mazao ya mifugo na samaki. Katika msimu huu, magonjwa kwa mifugo yanayoenezwa na kupe pamoja na wadudu warukao yanatarajiwa kupungua.
"Halikadhalika,kutokana na upungufu wa malisho na maji kuna uwezekano wa migogoro kujitokeza baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi."
Vile vile, Dkt.Ladislaus Chang’a amesema, uzalishaji wa zao la mwani unaweza kuathirika kutokana na vipindi virefu vya ukavu na joto vinavyotarajiwa.
"Jamii inashauriwa kuweka mpango mzuri wa matumizi na uhifadhi wa maji na malisho. Wafugaji na wavuvi wanashauriwa watumie taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani,"amesema Dkt.Chang’a.
Msimu wa mvua za vuli mahususi zitakuwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ikijumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, na Kilimanjaro, Pwani ya Kaskazini, Kaskazini ya Mkoa wa Morogoro.
Mikoa ya Pwani ikijumuisha Visiwa vya Mafia, Dar es salaam, Tanga na mikoa ya Ukanda wa Ziwa Victoria.
Dkt.Chang’a amebainisha kuwa, Kanda ya Ziwa Victoria mvua za mvuli zinatarajiwa kuwa wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ambapo zitaanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024 katika mikoa ya Geita.
Kagera na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na kutawanyika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2024.
Amesema kuwa,mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Desemba, 2024.
Vile vile amesema, mvua za vuli za wastani maeneo ya Pwani, Morogoro, Visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga na Visiwa vya Unguja na Pemba zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Desemba, 2024.
Aidha, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ambayo ni mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kutakuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani kuanzia wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Desemba, 2024.
Tags
Dr Ladislaus Chang’a
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Mvua za Vuli
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania