Wakili Sweetbert Nkuba kutinga mahakamani matokeo urais TLS

DODOMA-Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais wa chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Sweetbert Nkuba ametangaza kupinga matokeo mahakamani yaliyompa ushindi Wakili Boniface Mwabukusi huku akitaja sababu mbalimbali anazodai zimehujumu uchaguzi huo.
Akizungumza jijini Dodoma, Wakili Nkuba amesema hakubaliani na matokeo hayo na anapinga matokeo yaliyotangazwa na Kamati ya uchaguzi ya TLS kwasababu si matokeo yanayoakisi uchaguzi uliofanyika.

“Kuna uchakachuaji mkubwa sana umefanyika, Kamati ilikuwa ikijua idadi ya wapigakura wakati ikiandaa karatasi za kura lakini katika hali ya kushangaza na isiyo ya weledi.”

“Kamati ilishiwa karatasi za kupigia kura na Kamati ikachukua jukumu la kwenda kuchapisha karatasi nyingine katikati ya zoezi la uchaguzi, mnaweza kuona Kamati ilikuwa haijajipanga ama kwa makusudi au kwa kuamua kuhujumu jitihada ambazo tulikuwa tumezifanya katika kujiandaa na uchaguzi,”amesema.

Pia amesema walipeleka mawakala wa kuhesabu kura na makubaliano ilikuwa kwa namna yeyote wasipewe vifaa vya mawasiliano lakini katika hali ya kushangaza na yakustaajabisha matokeo yalianza kurushwa mitandaoni kabla ya kutangazwa na kamati ya uchaguzi.

“Wameanza kupongezana mitandaoni wakimpongeza mtu anayesadikika kuwa ni mshindi kabla matokeo rasmi hayajatangazwa na Kamati, matokeo yametangazwa masaa mawili kabla, na mshindi ameanza kupongezwa kwa maandiko mbalimbali kabla ya Kamati ya uchaguzi kutoa matokeo, tunaamini mawakala na watu wote waliokuwa kwenye chumba Cha kuhesabu kura hawakuwa na namna yeyote ya mawasiliano,”amesema.

Amesema uchaguzi huo umehujumiwa kutokana na Kamati kukosa weledi na kuhusika kuunajisi mchakato wa uchaguzi huo.

“Napenda kuujulisha umma ninakwenda mahakamani nimewaelekeza Mawakili wangu kwenda kupinga matokeo na kubatilisha ushindi uliotangazwa na Kamati ya uchaguzi,”amesema.

Wakili Nkuba amesema Mahakama ndio sehemu yenye haki na anaamini itasimamia haki na kuufuta uchaguzi huo na kuitisha uchaguzi mpya kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa viwango na kwa kuzingatia weledi na usawa wa pande zote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news