MWANZA-Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe.Jacobs Mwambegele amewataka wananchi wa maeneo ambayo Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unafanyika kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao mapema na kutokusubiri siku za mwisho ambazo mara nyingi huwa na foleni.
Jaji Mhe.Mwambegele amatoa wito huo Agosti 9,2024 mkoani Mwanza mara baada ya kufungua mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na wadau wa Uchaguzi uliofanyika katika ukumbi uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha,Jaji Mhe.Mwambegele amewatoa hofu wananchi ambao Kadi zao zinasomeka jina la Tume ya Uchaguzi na havina tatizo lolote, ama kuharibika au Kupoteza kuwa kadi hizo ni halali na zitaendelea kutumika bila tatizo lolote katika chaguzi zote zijazo.
Katika hatua nyingine Jaji Mhe.Mwambegele amewakumbusha wananchi kuwa kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa kisheria na adhabu yake yaweza kuwa faini au kifungo au vyote kwa pamoja.