ZANZIBAR-Waandishi wa habari nchini, wametakiwa kuielimisha jamii juu ya ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) hasa katika makundi yanayoonekana kuwa hatarini zaidi kupata ugonjwa huo endapo utaingia nchini.
Akitoa elimu ya ya ugonjwa huo kwa waandishi hao katika Ofisi ya Kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar,Menenja wa Kitengo hicho, Bakar Hamad Magarawa aliwataka wandishi hao kuielezea jamii dalili za ugonjwa huo pamoja na njia za kujikinga nao.
Alisema, ugonjwa huo unaosababishwa na kirusi cha Monkeypox uligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1958 nchini Denmark na kuenea katika nchi nyengine ikiwemo Jamhuri ya Demokrasia ya Congo kwa nchi za Afrika.
Alisema, maambukizi hayo yalianza kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu hasa katika nchi zilizokaribu na msitu wa mvua ya Kitropiki kusema kuwa, Zanzibar ipo hatarini kupata ugonjwa huo kutokana na mwingiliano wa wageni kutoka nchi tofauti.
“Mikoa mingine iliyo hatarini kupata ugonjwa huo kwa Tanzania ni pamoja na Katavi, Rukwa, Kigoma, Songwe, Mbeya, Dodoma na Dar es salaam,” alifafanua Meneja huyo.
Magarawa alisema, ugonjwa unapatikana kwa njia ya kujamiiana na mwenye maambukizi hasa mapenzi ya jinsia moja, kula au kugusa mizoga,kugusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa huo, kusalimiana kwa kukumbatiana, pamoja na kugusa majimamji ya mwili wa mtu mwenye maambukizi.
“Dalili za ugonjwa huo zinafanana na maradhi mengine, jambo ambalo ni gumu mtu kujitambua, licha ya ugonjwa huo kutokuwa na matibabu maalum bado jamii inashauriwa kuwahi kituo cha afya mara tu anapopata homa, vidonda vya koo,maumivu ya kichwa,maumivu ya mgongo,misuli,uchovu wa mwili, kuvimba kwa mitoki kuwashwa kwa muendelezo.
"Kupata upele, malengelenge, vidonda kwenye mwili hasa katika mikono, miguu kifua, uso na sehemu za siri dalili ambazo hujitokeza ndani ya wiki mbili baada ya kupata maambukizi,” alifahamisha Meneja huyo.
Siku za karibuni Waziri wa Afya Zanzibar,Nassor Ahmed Mazrui alinukulia na vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii akisema hakuna mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania licha ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuutaja ugonjwa kuwa ni janga la kiafya.
Alisema kutokana na kuripotiwa kwa ugonjwa huo katika nchi jirani za Kenya na Demkrasia ya Congo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kuchukua tahadhari za kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.
Alifahamisha kuwa, wizara imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa hasa katika viwanja vya ndege na bandarini kwa kufanya uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini, kutoa elimu kwa wahudumu wa afya na wananchi ya kuutambua ugonjwa huo na namna ya kujikinga.
Alisema, takwimu za siku za karibuni zinaonesha kuwa visa 38,465 na vifo 1,456 viliripotiwa kutoka Januari 2020 hadi Julai 2024 barani Afrika, ambapo virusi vya ugonjwa huo vinasambaa kwa kasi hasa katika nchi za afrika magaharibi na kati ambapo ugonjwa huo umeripotiwa kusambaa katika nchi 15 barani Afrika.
Miongoni mwa Waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo, Malik Sharan alisema mbali na elimu hiyo waliyoitoa kwao, alikiomba kitengo hicho kusambaza maofisa wa afya katika vyombo mbalimbali vya habari kutoa elimu ya ugonjwa huo ili jamii ipate uelewa zaidi juu ya ugonjwa huo.
“Sisi tutatoa habari tu na itaisha kwa siku moja lakini kukiwa na vipindi maalum katika vyombo tofauti itasaidia jamii kufahamu zaidi juu ya ugonjwa huu.”
Hafla hiyo iliandaliwa na Wizara ya Afya Zanzibar kupitia Kitengo cha Elimu ya Afya kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).