Watanzania kuanza kulipwa kupitia Facebook na Instagram, Dkt.Mwasaga asema 4R za Rais Dkt.Samia zimejibu

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Tehama (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga amevitaka vyombo vya habari nchini na watengeneza maudhui mitandaoni kutumia vema fursa ambayo inakuja ili kutengeneza maudhui mazuri ya Kiswahili yatakayochechemua uchumi wa kidigitali na kukuza mapato yao.
Dkt.Mwasaga ameyasema hayo leo Agosti 15, 2024 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati akifungua kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla mafunzo ya ulipwaji watengeneza maudhui kwenye mitandao ya kijamii ya Kampuni ya META (Facebook na Instagram).

Ni kwa wasanii,waandishi wa habari pamoja na waandaaji wa maudhui nchini.Ukiongozwa naa kauli mbiu ya "Fahamu fursa za kidigitali kwa maendeleo endelevu”

Mkutano huo umeandaliwa na Serikali kupitia Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Kampuni ya META (Facebook).

"Siku ya leo ni muhimu sana, hasa sisi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Baada ya kuingia madarakani Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alibainisha falsafa yake ya kuongoza nchi ya 4R au R4 kwa maana ya Reconcilation (Maridhiano), Resilience (Ustahamiliivu), Reforms (Mageuzi) na Rebuidlding (Kujenga Upya).
"Kwenye Sekta ya Habari na Utangazaji, falsafa hii ya 4R au R4 imetekelezwa kwenye Reforms. Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua hatua mbalimbali kuimarisha sekta ya habari na utangazaji nchini na nyie wote ni mashahidi.

"Kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika Sekta ya Habari na kukuwa kwa teknolojia kumekuwa na ongezeko kubwa la uwezeshaji, kukuza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja na kampuni mbalimbali."

Pia amesema, wingi wa vyombo vya habari vya mtandao unadhirisha uhuru wa kujieleza na uhuru wa kusambaza taarifa nchini.

"Kumekuwa na kampuni nyingi zinazotumia taarifa za mitandao kutoa huduma mbalimbali kwa jamii, kama mlivyosema mtandao unatoa fursa si kwa Tanzania tu bali unachokiandika kinapata fursa Dunia nzima.

"Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini jukumu kubwa la mitandao ya kijamii pamoja na mchango wao katika maendeleo ya Taifa letu.

"Kupitia mitandao ya kijamii tumeweza kuhabarisha wananchi kuhusu shughuli mbalimbali za Serikali na kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli mbalimbali."

Dkt.Mwasaga amefafanua kuwa,mitandao ya kijamii ni jukwaa pana ambalo linastawisha uchumi wa kidigitali kwa kasi, hivyo watengeneza maudhui hapa nchini wana nafasi kubwa ya kusonga mbele kiuchumi.

"Sababu kubwa ni kwamba,hii mitandao ya kijamii kama Meta. Sisi tunaona watumiaji wa Meta wapo zaidi ya bilioni 3.5 sasa kama Meta ingekuwa ni nchi,ninadhani ingekuwa ni nchi yenye watu wengi sana.
"Kwa hiyo, hii ni fursa kubwa sana, hii ni fursa kwa Tanzania, lakini pia ni fursa ya duniani kote."

Amesema, kutokana na ukubwa huo wa mitandao ya kijamii kama Meta, Instagram na Trending taifa linawategemea kwa asilimia kubwa watengeneza maudhui katika kuendeleza uchumi wa kidigitali nchini.

Pia amesema, kutokana na lugha ya Kiswahili kuendelea kusambaa kwa kasi duniani, hitaji la maudhui ya Kiswahili ni kubwa.

"Kwa hiyo maudhui ya Kiswahili yanahitajika,soko ni kubwa na watu wanataka kufahamu vitu vingi, hivyo majukwaa ya namna hii ndiyo yanaweza kuwafikia watu.

"Kwa hiyo mafunzo ya namna hii ni mafunzo ambayo yanahitajika sana ili kuweza kufanya uchumi wetu kuwa juu zaidi.

"Aidha,nimefurahi kusikia kuwa,Serikali kupitia Idara ya Maelezo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Meta ni waandaaji wa mkutano huu.
"Kitu kilichonifurahisha zaidi kwa sababu mahusiano tunayopenda kuyajenga sasa hivi ni mahusiano ambayo yanahusisha kampuni kubwa na muhimu sana katika uchumi wetu wa digitali, wadau wetu wa maendeleo kama UNESCO sisi wenyewe watu wa tume tuna mradi mkubwa sana tumekubaliana nao UNESCO wa kufundisha uchumi wa kidigitali."

Dhumuni la mkutano huo ni kukuza maarifa na ushirikiano kati ya Serikali,wadau wa maendeleo pamoja na asasi za kiraia.

"Lengo ni kubadilishana mawazo kuhusu kile tunachokipata kutokana na watu wanaotumia mitandao ya kijamii.

Aidha, ameeleza kuwa kutokana na ukuaji wa teknolojia ya habari ni muhimu vyombo vya habari vikawa na maarifa ya kutosha.

"Lengo ni kuwawezesha kutafsri habari na maudhui ambayo wanayapakia katika mitandao yao yaweze kujitosheleza kwa kukidhi vigezo vyote ili kuwapa walaji taarifa sahihi na za uhakika.
"Kuchanganua habari kwa ukamilifu na kufanya uamuzi sahihi na kushiriki kikamilifu katika mazungumzo ya umma kunaleta chombo chenye nguvu ambacho pamoja na mambo mengine kinatengeneza fikra muhimu zaidi katika enzi hizi za kidigitali.

"Aidha, mafunzo haya yatakuza ujuzi ambao utasaidia kujikinga na taarifa potofu ambazo zinachangia kuleta taharuki katika jamii inayohusika."

Kupitia ushirikiano wa kimkakati na mipango mbalimbali,Dkt.Mwasaga amesema,Serikali imekuwa ikishirikiana na UNESCO katika kuendeleza ujuzi kwa wana mtandao kama sehemu muhimu ya maendeleo endelevu ya Tanzania na ushiriki wa Kidemokrasia.

Aidha, UNESCO imelenga kuwawezesha watu binafsi kutengeneza mandhari ya kidigitali ipasavyo, kutengeneza taarifa za kidigitali na kuhuisha kwa kuchangia ipasavyo katika nchi na jumuiya mbalimbali.
"Usaidizi huu wa UNESCO umelenga kusaidia wananchi hasa vijana na wanawake na kuwapa teknolojia mbalimbali ambazo zitawasaidia kuweza kufanya shughuli zao kupitia teknolojia ya kidigitali ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

"Mnavyotumia mitandao ya kijamii ni vema mkajiendesha kama mnavyofanya nje ya mitandao kwani mitandao ni upanuzi wa hali ya hali yetu halisi ambayo tulikuwa nayo.

Pia, wamehimizwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuongeza ujuzi unaotakiwa ili kutengeneza maudhui mazuri ambayo yatawapa fursa ya kutengeneza kipato zaidi.

"Ni maudhui ambayo yatatusaidia kutengeneza uchumi wa kidigitali, kudumisha amani,"amesema Dkt.Mwasaga huku akiwasisitiza kuendelea kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazowaongoza.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa wa BASATA, Edward Buganga amewasihi wadau wa sanaa na watengeneza maudhui kutumia fursa ya mafunzo yanayotolewa kujiongezea ujuzi wa kuingiza kipato.

Mbali na kujiongezea kipato,Buganga amewataka kuandaa maudhui ambayo yatalinda utamaduni kupitia mitandao ya kijamii nchini.

Vile vile, Serikali imewataka waandaji maudhui kutumia zaidi lugha ya Kiswahili ili kutangaza nchi kimataifa.

Pia, wazingatie sheria na maadili ya kitanzania katika utengenezaji wa maudhui vile vile wafanye uchunguzi wa kina juu ya maudhui yao ili kuongeza ubora na tija katika maudhui yao.
Wakati huo huo, Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Dar es Salaam,Michael Toto amewataka walengwa wote kutumia fursa zilizopo katika mitandao ya kijamii ili kutengeneza kipato.

Amesema, uamuzi wa Meta kuanza kulipa maudhui ya Instagram na Facebook kwa watengeneza maudhui Tanzania ni hatua muhimu na wao UNESCO wataendelea kuwajengea uwezo ili kunufaika zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news