Waziri Kombo apokea mwaliko wa Rais Dkt.Samia kushiriki Jukwaa la FOCAC

DAR-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amepokea mwaliko rasmi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping utakaofanyika mwezi Septemba 2024 jijini Beijing nchini China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akimpokea Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Chen Mingjian alipofika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mwaliko huo umewasilishwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, pia umeainisha nafasi ya kipekee kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzungumza katika kikao cha ufunguzi kwa niaba ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na kuzungumza Katika Mkutano wa Ngazi ya Juu utakaojadili mada ya Maendeleo ya Viwanda na Kilimo cha Kisasa.

Akipokea mwaliko huo kwa niaba ya Mhe. Rais, Mhe. Balozi Kombo ameelezea kuwa nafasi ya Mhe. Rais kushiriki na kuzungumza katika Jukwaa hilo itaipa nchi fursa ya kuangazia uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla, hali ambayo itasaidia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania ni kinara na kiongozi wa kupigiwa mfano kwenye Jumuiya hiyo kongwe Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Chen Mingjian alipofika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Aidha,Balozi Kombo amemhakikishia Balozi Chen ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Kileke wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC ambapo Tamko la FOCAC na Mpango Kazi wa FOCAC itakuwa ni moja ya Matokeo ya Mkutano huo.

Naye Balozi wa China Mhe. Chen ameelezea kufurahishwa kwa China kutokana na kupokelewa kwa mwaliko wa kuhudhuria Mkutano na kuongeza kuwa kitendo hicho kinaendelea kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na China.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na ujumbe wake akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Chen Mingjian na ujumbe wake walipofika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Amesema China inaona Tanzania kama mshirika muhimu wa maendeleo kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla na kuahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania.

Jukwaa la Focac lilianzishwa kwa lengo la kukuza ushirikiano kati ya China na Afrika ili kuchagiza maendeleo kupitia sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo katika picha ya pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Chen Mingjian alipofika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na ujumbe wake katika picha ya pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Mhe. Chen Mingjian na ujumbe wake walipofika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

FOCAC limekuwa jukwaa linalotoa fursa sawa kwa pande zote mbili kujadili masuala muhimu ya kimaendeleo na kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia ikiwemo amani na usalama na mabadiliko ya tabia nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news