HARARE-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili Harare, Zimbabwe kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 13 na 14 Agosti, 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiongoza kikao cha ndani cha maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa SADC kilichofanyika tarehe 12 Agosti, 2024 katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Mkutano huo wa Mawaziri ni sehemu ya mikutano ya awali kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2024 nchini Zimbabwe.
Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu wa SADC kilichofanyika tarehe 8 hadi 11 Agosti, 2024 nchini humo ambacho kilijadili na kufanya maandalizi ya nyaraka mbalimbali zitakazo pokelewa na kujadiliwa na mkutano huo wa Mawaziri.
Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Balozi IGP (RTD) Simon Sirro wakifuatilia kikao hicho.
Kutoka kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Mratibu wa Masuala ya SADC Kitaifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri wakifuatilia kikao.
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadilino.
Mhe. Kombo akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe tarehe 12 Agosti, 2024.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe tarehe 12 Agosti, 2024.
Baada ya kuwasili nchini Zimbabwe, Mhe. Kombo amepokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Balozi IGP (RTD) Simon Sirro na kufanya kikao na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki katika mikutano ya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC.
Mawaziri wengine watakaoshiriki mkutano huo ni pamoja na; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW).