ARUSHA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa kazi kote nchini kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kutoa taarifa kwa wakati pindi wafanyakazi wanapoumia katika maeneo ya kazi ili waweze kupewa stahiki zao.
"WCF ina mchango na faida kwa wafanyakazi na waajiri katika kuhakikisha inatoa kinga ya kipato pindi majanga yasababishwayo na ajali, magonjwa au vifo kutokana na kazi," amesema.
Mhe. Waziri Ridhiwani Kikwete ametoa wito huo leo Agosti 30, 2024 jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha mfuko wa WCF na maafisa kazi kutoka mikoa ya Tanzania Bara ikiwa ni sehemu ya kuboresha utendaji kazi na kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi.
Aidha, Mhe. Ridhiwani amewataka maafisa kazi hao kusimamia sheria za kazi kwa kufanya kaguzi katika maeneo ya kazi ili kuhakikisha waajiri wanatekeleza matakwa ya sheria ya fidia kwa wafanyakazi.
Aidha, Mhe. Ridhiwani amesema serikali inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuzingatia masuala ya fidia kwa wafanyakazi sambamba na kuweka mazingira bora kwa waajiri ili waweze kutekeleza matakwa ya sheria ya fidia kwa wafanyakazi.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma alisema kwamba Mfuko umejizatiti katika kuhakikisha huduma zake zinapatikana kudijitali sambamba na kuimarisha ushirikiano na Idara ya Kazi kupitia maafisa kazi hao.
Naye Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa amesema, Idara ya Kazi imekuwa ikishirikiana na WCF ili kuhakikisha malalamiko ya wafanyakazi wanaoumia au kupata ugonjwa unaotokana na kazi zao yanatatuliwa kwa wakati.
Tags
Habari
Maafisa Kazi
Madhila Kazini
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)
Ridhiwani Jakaya Mrisho Kikwete
Ridhiwani Kikwete
Wafanyakazi
WCF Tanzania
Wizara ya Kazi na Ajira