Wizara ya Fedha yawashauri wananchi umuhimu wa kupanga bajeti ya fedha zao kwa ustawi bora kiuchumi

NA JOSEPHINE MAJULA
WF

WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na maeneo mengine ya Tanzania, wametakiwa kujenga mazoea ya kupanga bajeti ya fedha zao wanapouza mazao au kufanya biashara yoyote ili kuzitumia vizuri fedha hizo kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kujiongezea mitaji.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akigawa vipeperushi vyenye mada mbalimbali ikiwemo mikopo, akiba uwekezaji kwa baadhi ya wananchi wa Wilaya vya Ruangwa mkoani Lindi, waliojitokeza kupata elimu ya fedha.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Msimamizi Mkuu wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, wakati wa semina ya elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Lindi ambapo Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha ilifika kutoa elimu hiyo.
Baadhi ya wananchi wa Ruangwa, mkoani Lindi, wakisoma vipeperushi vyenye mada mbalimbali ikiwemo mikopo, akiba uwekezaji, walivyopewa na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha wakati wa semina ya elimu ya fedha mkoani Lindi.

“Tunatakiwa kutunza fedha tunazozipata katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji, ujasiriamali na biashara badala ya kuzifuja kwa kufanya matumizi yasiyo ya lazima yakiwemo sherehe na ngoma na kujikuta katika lindi la umaskini licha ya kupokea fedha nyingi katika shughuli zetu za kila siku,”alisema Bw. Kimaro.
Baadhi ya Wakazi wa Ruangwa, mkoani Lindi, walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakiangalia filamu yenye mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba, uwekezaji, na nyinginezo iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Lindi.

Aliiongeza kuwa mtu akijiwekea akiba itasaidia kujiepusha na mikopo “kausha damu” kwa kukopa fedha kwa watu wasio rasmi ambao hutoa fedha kidogo na kuwadai mazao mengi yasiyolingana na fedha walizokopeshwa.
Afisa Mchambuzi Hesabu Mwandamizi, kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Bi. Mariam Omari Mtunguja, akizungumza wakati wa semina ya utoaji elimu ya masuala ya fedha kwa Wakazi wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, ambapo mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo uwekezaji, mikopo na akiba.

Aidha, aliwasisitiza Wananchi wote nchini kuendelea kutunza fedha zao wanapozipata katika msimu uliopo na kutenga fedha kiasi kwa ajili ya kuhudumia shughuli za uzalishaji msimu unaofuata.
Mkazi wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Bi. Asteria Masanja, akiuliza swali kwa Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha iliyofika mkoani Lindi kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa Mkoa huo.

Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa elimu hiyo mkazi wa Ruangwa, Bi. Merryness Mutayabarwa, aliiomba Serikali kuona namna ya kutoa vifaa kama mitaji badala ya fedha taslimu ili viweze kuwasaidia katika shughuli za kiuchumi wanazofanya kama vile mashine za kutotolesha vifaranga, trekta na mifugo.

“Tukipatiwa fedha zinaweza kutumika vibaya tukashindwa kufanya marejesho kwa kuwa fedha ni rahisi mtu akiwa sio mwaminifu kubadili lengo la matumizi ya fedha hizo lakini tukipewa vifaa kama vile trekta, ng’ombe wa maziwa, mashine mbalimbali inakuwa rahisi kuzalisha na kutuwezesha kurudisha mitaji tuliyoazimwa kwa kuwa kunakuwa na uhakika wa kuzalisha”, alisema Bi. Mutayabarwa.
Afisa Maendeleo ya Jamii, Wilaya ya Ruangwa, Bw. Mwinyi Jalala, akiwashukuru Wananchi wa Ruangwa mkoani Lindi, waliojitokeza kupata elimu ya fedha iliyotolewa na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha ambapo mada mbalimbali zilifundishwa ikiwemo uwekezaji, mikopo na akiba.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ruangwa, Bw. Mwinyi Jalala, aliwasisitiza Wananchi wa Ruangwa wahakikishe wanapochukua mikopo wanarejesha kwa wakati ili kutoa fursa na wengine kupata fedha hizo za mikopo.
Baadhi ya Wakazi wa Ruangwa, mkoani Lindi, walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakiangalia filamu yenye mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba, uwekezaji, na nyinginezo iliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Lindi.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Lindi).

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Lindi katika Wilaya sita za Ruangwa, Liwale, Nachingwea, Mtama, Kilwa na Lindi Manispaa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news