Wizara ya Madini kuja na miradi mikubwa ya kimkakati

DODOMA-Wizara ya Madini kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali za uchimbaji na uchakataji madini inatarajia kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati itakayohusisha mnyororo mzima katika Sekta ya Madini.Hayo yamebainishwa leo Agosti 13, 2024 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini,Mhandisi Ramadhan Lwamo wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopaswa kutoa maeneo yao ili kuruhusu uendelezaji wa leseni za uchimbaji wa madini nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Mhandisi Lwamo amesema kuwa Tume ya Madini ilitoa Leseni za Uchimbaji wa Madini wa Kati na Mkubwa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo yamekuwa yakihitaji taratibu za kuhamisha wananchi ili kupisha utekelezaji wa miradi husika.

Aidha, Mhandisi Lwamo ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa uchimbaji madini ya nikeli wa Kabanga, Mradi wa uchimbaji mkubwa wa SMCL mkoani Mwanza, Mradi wa uchimbaji madini ya Kinywe wa Faru Graphite mkoani Morogoro, Mradi wa uchimbaji madini ya mchanga mzito wa Baharini (Heavy mineral sands).
Vilevile, Mhandisi Lwamo ameitaja miradi mingine ni pamoja na Mradi wa uchimbaji madini ya Kinywe wa Bunyu, Nachu na Chilalo mkoani Lindi na Epanko mkoani Morogoro.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Wizara ya Madini inaahidi kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha Kampuni zinakamilisha taratibu za ulipaji wa fidia kwa wananchi pamoja na kuendeleza miradi husika na kusimamia utekelezaji wake.
Waziri Mavunde ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa ushauri wake makini ambao imekuwa ikiutoa katika nyakati tofauti na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri wote wa Kamati hiyo katika kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kukua kwa kasi na hatimaye kuchangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news