Wizara ya Madini yaanza utekelezaji wa Programu ya Wanawake na Vijana (MBT) kwa vitendo

SHINYANGA-Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ameeleza kuwa Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kusaidia wachimbaji wanawake na vijana (Mining For A Brighter Tomorrow-MBT) kwa lengo la kuwainua kiuchumi.Ameyasema hayo Agosti 10, 2024 katika Kijiji cha Nyamishiga, Halmashauri ya Msalala aliposhiriki hafla ya utoaji wa leseni za uchimbaji mdogo 4 kwa kikundi cha wakina Mama cha TAWOMA Mshikamano.

"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anayo dhamira ya kweli ya kuwawezesha na kuwainua wachimbaji wadogo hususan wanawake na vijana na ndiyo maana amenipa maelekezo mahsusi ya kuwahudumia, kuwawezesha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Mhe. Rais ni mdau namba moja wa wachimbaji wadogo nchini," alisema Mhe. Mavunde.
Aliongeza kwamba Wizara utaendelea kutoa Leseni kwa wachimbaji wadogo nchini na kuwapanga vizuri ili kuchochea ukuaji wa sekta ya Madini.

"Niwapongeze kikundi cha Mshikamano kwa kurudisha kwa Jamii (CSR) kupitia ujenzi wa Zahanati,Manunuzi ya gari la Wagonjwa na ujenzi wa nyumba za watumishi wa Afya,matumaini yangu ni kwamba mtafanya vizuri zaidi baada ya kuwakabidhi Leseni hizi," alisema.

Aliongeza kuwa, Serikali itaendelea kushughulikia suala la upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika na uboreshwaji wa miundombinu ya barabara katika eneo hilo na kueleza. "niendelee kukumbusha juu ya upunguzwaji wa tozo nyingi za Halmashauri kwa wachimbaji wadogo kama ambavyo iliridhiwa katika mkutano uliopita ulioshirikisha viongozi wa Halmashaur".

Akitoa salamu kwa niaba ya wanakikundi cha Mshikamano, Mwenyekiti Wa TAWOMA Taifa, Semeni Malale Mwenyekiti alimshukuru,Mhe. Rais kwa namna anavyoendelea kuwajali wachimbaji wadogo hususan wanawake na vijana na kuahidi kwamba watakwenda kufanya shughuli za uchimbaji kwa kufuata taratibu zote na kulipa maduhuli ya Serikali kama inavyotakiwa ili kuchangia mapato.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mhe. Idd Kassim alieleza kufurahishwa na namna Serikali inavyoshughulikia changamoto za uchimbaji na kuiomba Serikali kuweka mkazo katika kuharakisha kufanya utafiti wa madini ili wachimbaji wawe na taarifa sahihi yalipo madini.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita alionesha wazi furaha yake na kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kuwainua wachimbaji wanawake na vijana kiuchumi, na kuahidi kuwa ataendelea kuwapa ushirikiano wachimbaji wote ili wafanye shughuli zao kwa ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news