DODOMA-Imeelezwa kwamba kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2022 hadi Agosti 2024 , Wizara ya Madini imeendelea kuratibu na kusimamia Masuala yanayohusu Usalama Mahali pa kazi pamoja na afya za wafanyakazi katika migodi ikiwemo UKIMWI , Kifua Kikuu na magonjwa sugu.


Akielezea kuhusu mkakati wa Wizara Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema, Wizara inaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mkakati wa masuala ya UKIMWI na magonjwa yasioambukizwa katika migodi mikubwa na ya Kati ili kupunguza maambukizi mapya na kuimarisha nguvu kazi ya wafanyakazi na jamii kama mkakati wa sekta ya madini unavyoelekeza kuhusu kudhibiti maambukizi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Magonjwa sugu.

Dkt.Kiruswa ameongeza kuwa, ili kuendelea kupambana na maambukizi ya VVU na magonjwa sugu, Wizara itaendelea kushirikiana na taasisi binafsi zinazoshughulika na afya kubuni mbinu mpya rafiki katika kutoa elimu ya afya na kuzikumbusha kampuni za uchimbaji madinib ziendelee kuchangia mfuko wa kupambana na maradhi.
Kwa upande wake , Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI , Bernadetha Mshashu ameipongeza Wizara ya Madini kwa kazi nzuri inayofanya ikiwa pamoja na kutekeleza maagizo yanayotolewa na Kamati kuhusiana na ujumuhishaji wa jamii ndani na nje ya migodi katika kutoa elimu ya afya.
Akizungumza kwa niaba mgodi wa Uchimbaji dhahabu Geita (GGM) Daktari Aalen Mtemi amesema, mgodi wa GGM unatambua umuhimu wa afya ya mfanyakazi mahali pa kazi hivyo katika kipindi husika imeweza kuchangia shilingi bilioni 1.75 katika Mifuko ya Kupambana na Maradhi yasioambukizwa na yanayoambukizwa.
