WMA yawapongeza wakulima Karatu kwa kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi

NA VERONICA SIMBA
WMA

KAIMU Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Albogast Kajungu, amefanya ziara ya kushtukiza katika mashamba ya wakulima mbalimbali eneo la Mang’ola wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha na kuridhishwa na namna wakulima hao wanavyozingatia matumizi ya vipimo sahihi.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) Albogast Kajungu (kulia) akiongoza zoezi la kuhakiki uzito wa vitunguu vilivyofungashwa tayari kwa kuuzwa katika eneo la Mang’ola wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, Agosti 9, 2024. WMA ilifanya ziara ya kushtukiza ili kujiridhisha endapo maelekezo ya Serikali kwa wakulima na wafanyabiashara kutozidisha kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa ili kulinda pande zote, yanazingatiwa.

Akiongoza Timu ya Wataalamu wa WMA katika zoezi hilo, Agosti 9, 2024, Kajungu amesema lengo ni kujiridhisha ikiwa wananchi wanazingatia elimu inayotolewa na Wakala wa Vipimo kuhusu matumizi ya vipimo sahihi ili kuzilinda pande zote yaani wakulima, wafanya biashara na walaji.

Katika ziara hiyo, Timu hiyo ya Wataalamu wa WMA walihakiki uzito wa mazao aina ya vitunguu yaliyofungashwa katika vifungashio vya aina mbalimbali tayari kwa kuuzwa pamoja na kuzungumza na wakulima, wafanyabiashara na wasafirishaji wa mazao hayo.

“Niwapongeze sana kwa kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi maana katika mazao yote yaliyofungashwa ambayo tumepima, hakuna yaliyozidi uzito unaoelekezwa kisheria. Nawasihi muendelee hivyo kwani kila upande utapata faida stahiki,” amesema Kajungu.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) Albogast Kajungu (kulia) akiongoza zoezi la kuhakiki uzito wa vitunguu vilivyofungashwa tayari kwa kuuzwa katika eneo la Mang’ola wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, Agosti 9, 2024. WMA ilifanya ziara ya kushtukiza ili kujiridhisha endapo maelekezo ya Serikali kwa wakulima na wafanyabiashara kutozidisha kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa ili kulinda pande zote, yanazingatiwa.

Akifafanua zaidi kuhusu maelekezo ya kisheria kwa uzito wa mazao ya shamba yaliyofungashwa, Kajungu amesema mkulima yuko huru kufungasha kwa kutumia aina yoyote ya kifungashio isipokuwa azingatie uzito wake usizidi kilo 100.

Ametoa ufafanuzi huo kutokana na uelewa tofauti kwa baadhi ya watu wanaotafsiri kuwa sheria inakataza kufungasha mazao kwa kuongeza kishungi katika vifungashio.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) Albogast Kajungu (kulia) akimpongeza Mfanyabiashara wa Vitunguu katika eneo la Mang’ola wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, Felix Matle kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali kwa wakulima na wafanyabiashara kutozidisha kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa ili kuzilinda pande zote. Wataalamu wa WMA, walifanya ziara ya kushtukiza katika eneo hilo, Agosti 9, 2024 ili kujiridhisha endapo maelekezo husika yanazingatiwa.

“Niendelee kuwaelimisha na kuwaelewesha kuwa tafsiri sahihi ya lumbesa siyo kishungi bali ni uzito uliozidi kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa, Na katika hili niseme wazi huwezi kuthibitisha lumbesa kwa macho, ni lazima upime kujiridhisha kuwa mazao yaliyofungashwa yamezidi kilo 100,” amesisitiza Kajungu.

Katika hatua nyingine, Kajungu ameendelea kutoa ushauri kwa Halmashauri zote nchini kutumia mizani kupima mazao yaliyofungashwa ili kuondoa utata na manung’uniko yanayojitokeza kwa baadhi ya wakulima na wafanyabiashara kwamba wanatozwa faini kwa mazao yaliyofungashwa na kuwa na kishungi yakitafsiriwa kama lumbesa.

“Mwarobaini wa changamoto hiyo ni kutumia mizani kama sheria inavyoelekeza na siyo kutizama kwa macho.”
Wataalamu wa Wakala wa Vipimo (WMA), wakiwa katika eneo la Mang’ula wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha kuhakiki vitunguu vilivyofungashwa tayari kwa kuuzwa. WMA ilifanya ziara ya kushtukiza Agosti 9, 2024 ili kujiridhisha endapo maelekezo ya Serikali kwa wakulima na wafanyabiashara kutozidisha kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa ili kulinda pande zote, yanazingatiwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima na wafanyabiashara wa vitunguu katika eneo la Mang’ola wamekiri kunufaika zaidi kwa kila upande baada ya kuanza kuzingatia elimu ya vipimo sahihi waliyopatiwa na Serikali kupitia Wakala wa Vipimo.

Marieta Tlemai, mkulima wa vitunguu, kwa niaba ya wenzake, ametoa pongezi kwa Serikali kupitia Wakala wa Vipimo kwa kuwajali wakulima na kuweka sheria ya ufungashaji mazao inayolenga kulinda maslahi yao.
Vitunguu vilivyofungashwa vikipimwa katika mzani wakati wa zoezi la kuhakiki mazao yaliyofungashwa eneo la Mang’ula, wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha. Wakala wa Vipimo (WMA) ilifanya ziara ya kushtukiza katika eneo hilo Agosti 9, 2024 ili kujiridhisha endapo maelekezo ya Serikali kwa wakulima na wafanyabiashara kutozidisha kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa ili kulinda pande zote, yanazingatiwa.

Awali, timu hiyo ya Wataalamu kutoka WMA, ilitembelea Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu ili kueleza dhamira ya ziara yao na kupokelewa na Katibu Tawala, Dkt. Lameck Karanga ambaye aliwahakikishia kuwa Ofisi yake inaunga mkono jitihada za kutokomeza lumbesa ili kulinda maslahi ya wananchi wake ambao wengi hujishughulisha na kilimo cha vitunguu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news