Yanga SC yaichapa Kagera Sugar mabao 2-0, KMC vs Coastal Union zatoka sare huku Fountain Gate FC ikiwachapa Namungo FC mabao 2-0

NA DIRAMAKINI

MABINGWA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Young Africans Sports Club wameanza utetezi wa ubingwa huo kwa msimu wa 2024/2025 baada ya kuwachapa Kagera Sugar mabao 2-0.
Kagera Sugar iliwaalika Yanga SC kwenye uwanja wa Kaitaba saa 11:00 jioni ya Agosti 29,2024 ukiwa ni mchezo wa pili kwao na wa kwanza kwa wageni hao.

Ni baada ya Yanga SC kurejea kutoka kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika ambapo katika hatua za awali imevuna alama sita na mabao 10.

Dakika ya 26 ya kipindi cha kwanza, Maxi Mpia Nzengeli alianza kulipa bili ya mwajiri wake kwa kutupia bao safi ambalo lilidumu hadi mapumziko.

Licha ya Yanga SC,kuwa na nafasi ya kupata mabao mengi zaidi kupitia mtanange huo, mambo hayakwenda vema, lakini Clement Mzize dakika ya 88 aliongeza bao la pili.

Hadi mtanange huo unafikia tamati, ubao ulikuwa unasoma mabao 2-0, hivyo kuifanya Yanga SC kuanza vema safari yao katika ligi hiyo yenye timu 16.

KMC vs Coastal Union

Mchezo wa kwanza ulipigwa saa 10:00 Alasiri kati ya KMC na Coastal Union kwenye uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Aidha,mchezo huo ni wa kwanza kwa timu zote mbili katika msimu huu ambapo dakika ya 33,Ibrahim Ilyas Ahmed alianza kuiandikia KMC bao la kwanza.

Ni bao ambalo lilidumu mpaka kipindi cha pili dakika ya 86 ambapo Maabad Maulid alisawazisha, hivyo hadi tamati ubao ukasoma sare ya bao 1-1.

Namungo FC vs Fountain Gate FC

Katika mchezo wa mwisho Agosti 29,2024 uliozikutanisha Namungo FC dhidi ya Fountain Gate FC katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, wenyeji wamekubali kichapo cha mabao 2-0.

Mchezo huu ulitakiwa kuchezwa hapo awali, lakini uliahirishwa baada ya Fountain Gate kuwa na changamoto za usajili.

Aidha, matokeo hayo yanaifanya Namungo FC kuwa na mwenendo usioridhisha kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, baada ya awali kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka Tabora United FC.

Mabao ya Fountain Gate FC yamefungwa na Edgar William dakika ya 30' huku dakika ya 45', Seleman Mwalimu akifunga hesabu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news