Yanga SC yaichapa Red Arrows mabao 2-1 Agosti 8 watafika?

NA GODFREY NNKO

MABINGWA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara,Young Africans Sports Club (Yanga SC) ya jijini Dar es Salaam imeendelea kuonesha ukubwa wao baada ya kuonesha kandanda safi kupitia Siku ya Mwananchi leo Agosti 4,2024.
Ni baada ya kuutumia vema Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam kwa kuachia kichapo cha mabao 2-1 kwa wageni wao Red Arrows kutoka Lusaka nchini Zambia.

Kupitia mtanange huo wa kirafiki ambao mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Philip Isdory Mpango kwa mara ya kwanza viwanja viwili kwa maana ya Benjamin Mkapa Stadium na Uhuru Stadium vyote vimejaa mashabiki.

Ricky Banda alianza kuvuruga tabasamu la maelfu ya mashabiki wa Yanga SC baada ya kutundika bao ndani ya dakika sita. Bao ambalo lilidumu hadi kipindi cha kwanza cha dakika 45 kutamatika.
Aidha, baada ya ukimya huo kwa wenyeji wenye shughuli yao, Yanga SC ndani ya dakika ya 62, Mudathir Yahya Abbas alisawazisha bao la Red Arrows.

Hapa, tabasamu la Wananchi likaanza kuonekana tena ambapo Aziz Ki ndani ya dakika 90' alifunga mjadala kwa bao safi la penalti.
Awali, uongozi wa Yanga SC ulisema watalipa kisasi cha mtani wao wa jadi Simba SC kwa kuonesha ukubwa walionao.

Ni baada ya Agosti 3,2024 wakati wa Simba Day, klabu ya Simba kufanya kweli kwa kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe usiku wa kuamkia Agosti 4,2024 alikuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na kubainisha kuwa,

“Wameanza wenyewe sasa sisi tunakwenda kumaliza tunataka kuandika rekodi ikifika saa sita mchana mageti ya Uwanja wa Mkapa yafungwe,maana tumeona wenzetu mpaka saa 10 jioni bado mageti yalikuwa wazi,lakini sisi tunakwenda kuandika rekodi ambapo tutatumia na Uwanja wa Uhuru pia.”
Kwa Young Africans Sports Club, pengine mechi hii dhidi ya Red Arrows ni kipimo muhimu kwao katika kujiandaa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC pamoja na michuano mingine.

Ikumbukwe Red Arrows, ambao ni mabingwa wa Kombe la Kagame 2024, ni timu yenye uwezo mkubwa na imetoa changamoto kubwa kwa Young Africans Sports Club.
Wiki ya Mwananchi ambayo imefikia kilele leo huwa inajumuisha matukio mbalimbali yanayohusisha klabu hiyo na mashabiki wake ikiwemo kujitoa kwa jamii mbalimbali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news