Young Africans Sports Club yaichapa Vital'O FC mabao 4-0

NA DIRAMAKINI

MABINGWA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Young Africans Sports Club ya jijini Dar es Salaam imeanza vema Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Ni baada ya kutwaa alama tatu ambazo zinaambatana na mabao 4-0 dhidi ya Vital'O FC ya Burundi kwenye mchezo wa hatua ya awali.

Mtanange huo umepigwa Agosti 17,2024 katika dimba la Chamazi Complex lililopo Kata ya Chamazi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam.

Nyavu za Warudi zilianza kufumaniwa na mshambuliaji wa Kimataifa wa Zimbabwe, Prince Dube dakika ya tano katika kipindi cha kwanza ambalo lilidumu hadi mapumziko.

Licha ya tambo za awali za Warudi ambao walikuwa wenyeji katika dimba hilo, kipindi cha pili Clotous Chama dakika ya 68 aliwasimamisha tena mashabiki wa Yanga.

Dakika ya 74, Clemence Mzize alitupia bao la tatu ambalo lilizidi kuwapa raha zaidi kabla ya Stephanie Aziz Ki ajahitimisha bao la nne dakika ya 90 kwa mkwaju wa penalti.

Mchezo wa marudiano Agosti 24,2024 utaamua timu itakayokata tiketi ya hatua ya kwanza ambapo Young Africans Sports Club watakuwa wenyeji.

Vital’O imekuwa mwenyeji wa mchezo huu, Yanga ikicheza kama mgeni katika mzunguko wa kwanza.

Aidha,mchezo unachezwa Dar es Salaam kutokana na viwanja vya Burundi kutokidhi vigezo kwa mujibu Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news