NA GODFREY NNKO
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Young Africans Sports Club (Yanga SC) ya jijini Dar es Salaam wametwaa Ubingwa wa Ngao ya Jamii 2024.
Ni baada ya kumenyana na Azam FC katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam leo Agosti 11,2024.

Bao hilo, lilionekana kuwatia hasira Yanga SC ndipo Prince Dube dakika ya 19 ya kipindi cha kwanza akasawazisha.

Kama walivyowahi kusema Waswahili kuwa, kutangulia si kufika hayo yalitimia kwa Azam FC ambao walitangulia kufunga, lakini hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza kinatamatika, Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 3-1.
Clement Mzize ndiye aliyezamisha jahazi la Azam FC dakika ya 90' baada ya kuzifumania tena nyavu zao ambapo hadi mtanange huo unaisha matokeo yalikuwa Yanga SC mabao 4 huku Azam FC wakiambulia moja.
Ushindi huo, unaiwezesha Yanga SC kutwaa ubingwa wa nane wa Ngao ya Jamii tangu michuano hiyo ilopoanza mwaka 2001 huku watani zao Simba SC wakiwa wameitwaa mara 10.
Simba SC vs Coastal Union
Awali katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa Ngao ya Jamii kati ya Simba dhidi ya Coastal Union uliopigwa hapo hapo Benjamin Mkapa umemalizika kwa Simba SC kupata ushindi wa bao moja.
Saleh Karabaka aliwapatia Simba bao hilo pekee dakika ya 11 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Joshua Mutale.

Kipindi cha pili Coastal walirudi kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Simba SC bila mafanikio.
Aidha,kiungo mkabaji Fabrice Ngoma alitolewa dakika ya 84 baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano kufuatia kumchezea madhambi Mbaraka Yusuph wa Coastal Union.