Young Africans Sports Club yaidhalilisha Vital’O FC kwa mabao 10-0

NA DIRAMAKINI

MABINGWA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Young Africans Sports Club (Yanga SC) ya jijini Dar es Salaam wametinga raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Ni baada ya ushindi wa jumla ya mabao 10-0 dhidi ya Vital'O FC kutoka nchini Burundi katika mchezo wa hatua ya awali.

Yanga SC na Vital’O FC zimeumana katika mchezo wa marudiano Agosti 24,2024 katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamazi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam.

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzou ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao hayo baada ya dakika ya 14' kipindi cha kwanza kuzifumania nyavu za Vital’O.

Naye Clement Mzize alitupia bao la pili katika dakika ya 49 ya kipindi cha pili cha mtanange huo, huku dakika ya 51 kiungo, Clatous Chota Chama akipachika bao la tatu.

Prince Dube dakika ya 72 alichomeka msumari mwingine, na Stephanie Aziz Ki akagonga mwingine dakika ya 78.

Huku, Vital’O wakiendelea kutafakati kuhusu kipi kimewasibu, dakika ya 86 Mudathir Yahaya Abbas alipachika bao la sita.

Hadi dakika 90 zinatamatika ubao ulikuwa unasoma Young Africans Sports Club mabao 6 huku Vital’O ubao ukisoma 0.

Yanga imeshinda mechi zake kwa jumla ya mabao 10-0 baada ya kuizaba Vital’O mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza Agosti 17,2024 katika dimba hilo.

Aidha, mchezo ujao itamenyana na Benki ya Biashara ya Ethiopia (CBE SA) kwenye raundi ya kwanza kutafuta tiketi ya hatua ya makundi ya CAFCL 2024/25.

Ni baada ya CBE SA kutoka sare ya bao 1-1 na Villa SC, na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2.

Waethiopia hao waliwazaba Waganda mabao 2-1 wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Sazza Grounds huko nchini Uganda wiki iliyopita katika mechi ya kwanza.

Hata hivyo, baada ya mtanange huo,Msemaji wa Vital’O FC, Arsene Bucuti amekiri kuwa, Yanga SC ni timu bora zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Pia, amesema kucheza na Yanga ni kama kuacha kusoma shule ya msingi na kwenda shule ya sekondari huku akiwashukuru Watanzania kwa mapokezi mazuri tangu walipoingia hapa nchini.

Ushindi huo wa mabao 10 umeiwezesha Young Africans Sports Club kuchukua shilingi milioni 50 za hamasa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news