Zanzibar yasaini mkataba na Potential Builders Limited ujenzi miundombinu ya umeme wa jua

ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeisainisha mkataba Kampuni ya Potential Builders Limited kutoka Tanzania Bara kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mradi wa umeme wa jua.
Waziri wa Maji Nishati na Madini Shaib Hassan Kaduwara (aliyesimama kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Nishati na Madini, Joseph Kilangi wakishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Jua katika Kijiji cha Makunduchi Zanzibar baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Potential Builders Ltd kutoka Dar es Salaam ambapo zaidi ya shiling bilioni 9 zinatarajiwa kutumika.Kulia anayesaini ni Meneja Mkuu Shirika la Umeme Zanzibar,Haji Haji na  Mhandisi David Mwasomola kutoka kampuni hiyo,hafla hiyo ilifanyika ofisi za ZURA Maisara Zanzibar.

Utiaji saini huo ulifanyika huko Maisara katika jengo la ZURA kwa upande wa Serikali aliyesaini mradi huo alikuwa ni Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar,Haji Haji na kwa upande wa kampuni hiyo alikuwa Mhandisi David.A. Mwasomola.

Waziri wa Maji, Nishati na Madini,Mhe, Shaibu Hassan Kaduwara alisema,mradi huo utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya kukatika kwa umeme katika visiwa vya Zanzibar.

Alisema kuwa, itakuwa vyema mradi huo ukamalizika kabla ya miezi sita ya makubaliano.

Aliitaka kampuni hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili kumalizika mradi kwa wakati.

Aidha,alilitaka Shirika la Umeme kuwa karibu na kampuni hiyo kwa usimamizi na ufuatiliaji mwenendo mzima wa ujenzi.
Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Haji Haji (mwenye koti) akipeana mikono na kubadilishana hati za mkataba huo na Mhandisi David Mwasomola wa Kampuni ya Potential Builders Ltd.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph Kilangi alisema, mradi huo unajengwa kwa pesa za mkopo kutoka Benki ya Dunia na utakagharimu zaidi ya shiligi Bilioni 9 ambao ujenzi wake utaanzia usafishaji wa maeneo ya ujenzi wa barabara za ndani na sehemu za kuhifadhia mitambo.

Alisema, umeme huo wa Megawatts 18 utajengwa katika maeneo ya Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news