ZANZIBAR-Chama cha ACT Wazalendo kimemkabidhi gari aina ya Prado, Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Juma Duni Haji ikiwa ni sehemu ya kutekeleza Sera yao ya kuwaenzi viongozi wastaafu.
Babu Duni amezawadiwa pia zawadi mbalimbali na viongozi wa Kitaifa, mikoa na majimbo.
Ni kupitia hafla hiyo ya kumkabidhi gari ambayo imefanyika Septemba 4,2024 jijini Zanzibar.
Aidha,viongozi mbalimbali wa ACT Wazalendo wamehudhuria akiwemo Kiongozi wa chama, Doroth Semu, Mwenyekiti wa Chama Taifa ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Otham Masoud Othman,
Makamu wenyeviti wa Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Mkuu pamoja na mamia ya wanachama wa ACT Wazalendo.
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu akizungumza kwenye hafla hiyo ya kusherehekea maisha ya utumishi ya Mwenyekiti mstaafu Babu Duni amesema;
"Siku ya leo siyo siku ya kawaida katika historia ya chama chetu. Siku ya leo ni siku yenye upekee mkubwa sana.
"Siku ya leo tunatoa majibu kwa vitendo kwamba ACT Wazalendo ni chama cha kiungwana, chama kinachojali na ni chama kinachotekeleza siasa safi ndani na nje ya chama."Sera imeweka utaratibu wa kuwajali, kuwaangalia, na kuwatunza viongozi wakuu wastaafu na imeweka mazingira ya namna mbili, wapo viongozi wawili wametajwa kwenye sera ile, Kiongozi wa chama mstaafu, na Mwenyekiti wa chama mstaafu, hawa ni lazima kuwaangalia, kuwajali na kuwatunza.
"Na zipo stahiki zimewekwa kwenye sera ile na inasema iwapo kiongozi wa chama mstaafu na mwenyekiti wa chama mstaafu watakuwa hawana makazi ni wajibu wa chama kuhakikisha wanapata makazi.
"Na iwapo watakuwa hawana usafiri unaoendana na hadhi ya Kiongozi wa chama mstaafu na mwenyekiti wa chama mstaafu ni wajibu wa chama kuhakikisha viongozi hawa wanapata usafiri, na sera inasema tuwaangalie pia kwenye matibabu na mambo mengine ya kimaisha."