Agizo la Waziri Aweso larejesha huduma ya maji Mbokomu

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) imetekeleza Agizo la Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb) la kuhakikisha huduma ya maji inarejea kwa wakazi wa Kata ya Mbokomu ifikapo Septemba 2,2024.
Mamlaka imetekeleza agizo hilo kwa kuhakikisha miundombinu ya majisafi iliyoharibiwa na mafuriko imerejeshwa.

Mamlaka kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 ilitenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya miundombinu inayojumuisha bomba za maji zenye urefu wa mita 700.

Sambamba na ukarabati wa chanzo cha maji cha Chemichemi ya Mrusunga kilichopo kwenye Kata ya Mbokomu mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza urejeshaji wa huduma hiyo, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Mbokomu, Stella Mrema amesema, wanaishukuru Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Moshi kwa jitihada za haraka, kwani sasa huduma imerejea na wananchi wanafurahia, kwani hakuna changamoto katika eneo lao.

"Kuhusiana na changamoto ya maji Kata ya Mbokomu ambayo ilikuwepo kuanzia mwezi wa tano, kwa sasa tunaishukuru sana Mamlaka ya MUWSA ya Moshi Mjini imejitahidi kama alivyoahidi Mkurugenzi kuwa tarehe mbili maji yangekuwa yametoka na kweli usiku wa tarehe mbili maji yalitoka na mpaka sasa hivi maji yapo mengi kabisa. Mabomba mengine yanapasuka.

"Kwa hiyo zile kelele za kila siku wananchi walikuwa wanapiga simu kuwa jamani changamoto moja ya maji mbona hamna, sasa hivi sijasikia kelele yoyote ya wananchi kwa hiyo tunawashukuru sana kwa kweli wamepambana maji yapo."
Ameeleza kuwa, wakati wa changamoto ya maji awali yalikuwa ya mgao kwani yalikuwa yakitoka kidogo,hivyo kusababisha mabomba ya ndani na vyoo vya ndani kutotumika.

"Lakini kwa sasa, baada ya mamlaka kurekebisha maji ni mengi na wanayatumia kwa matumizi mbalimbali."

Wananchi wa Kata ya Mbokomu walipata kadhia ya kukosa huduma kwa miezi kadhaa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha Mkoani Kilimanjaro kuharibu miundombinu ya Majisafi.

James Samwel wa Mbokomu anasema kuwa, "hali ya sasa hivi ni nzuri, tunapata maji, hatupati shida tena na hatunywi maji ya mfereji.

"Tulikuwa tunakunywa maji ya mfereji, lakini kuanzia tarehe mbili, hatunywi maji ya mfereji hapa nina|tuna furaha sijui nisemeje."

Samwel anafafanua kuwa, maji safi na salama ni hitaji lao muhimu katika maisha ya kila siku, hivyo hatua hiyo ya kupatiwa maji ya bomba ni furaha kubwa kwao.

Amesema, kwa upatikanaji huo wa maji safi hakutasikika malalamiko tena kutoka kwao, kwani sasa huduma ya maji ni uhakika.

Kwa upande wa wanawake wa Mbokomu wamesema kuwa, awali walikuwa wakipitia kipindi kigumu wakati wa kwenda kutafuta maji kwa matumizi ya nyumbani na kufulia.

"Awali tulibeba mandoo, makarai kwenda kufua huko mtoni,vitoto vilichoka. Saa nyingine tulilala njaa na chakula tunacho, kwa sababu hatuna maji ya kupikia, kwa hiyo tunawashukuru mno na hatuna hata neno linalotosha kuwashukuru Serikali yetu na nyinyi watoto wetu.

"Mwanzo maji hayakuwepo kwenye bomba kweli, tulikuwa tunateseka sana tunaenda mpaka huko kwenye mfereji, lakini asubuhi nimechota maji na sasa hivi nimechota maji, kwa hiyo sasa hivi mabomba yanatoa maji mengi sana tunaishukuru sana Serikali na Mungu awabariki."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news