Ahadi ya Rais Dkt.Samia ujenzi wa kiwanda cha chumvi yaanza kutekelezwa

LINDI-Waziri wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Ujenzi wa Kiwanda cha kusafisha madini ya chumvi kinachojengwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika eneo la Lingaula Wilayani Kilwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa wakulima wa chumvi alipofanya ziara yake mkoani Lindi.
Amebainisha hayo leo Septemba 18, 2024 alipotembelea eneo patakapojengwa kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na kupokea rasmi Hati ya umiliki wa ardhi wa eneo hilo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Mhe. Mavunde amesema kuwa, anamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha wakulima wa chumvi juu ya ukosefu wa masoko ya uhakika, hatua iliyopelekea kutupa maelekezo ya kuhakikisha tunasimamia ujenzi wa kiwanda hiki haraka ili kutatua kero hiyo ya muda mrefu kwa wakulima wa chumvi wa maeneo mengi nchini ikiwemo wa Mkoa wa Lindi.

“Mhe. Rais alipokuja kwenye ziara yake katika Mkoa huu, moja kati ya mambo aliyoyasikia na kupokea ni kilio cha Wazalishaji wa Madini ya Chumvi na akaagiza kiwanda cha chumvi kijengwe hapa, na niwaambie kuwa Mhe. Rais anafuatilia suala hili la wazalishaji wa chumvi na hatua hii ni utekelezaji wa ahadi yake kwenu baada ya kusikia kilio chenu"

“Rais wetu anayodhamira ya dhati ya kuwanyanyua wazalishaji wa madini ya chumvi ili waweze kupiga hatua, kama ilivyo kwa wachimbaji wa madini mengine nchini,” amesisitiza Mhe. Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde ameiagiza STAMICO kuhakikisha kabla ya Mwezi wa Disemba, 2024 wanafanya mafunzo ya namna bora ya kulima chumvi ili waweze kuzalisha chumvi yenye ubora unaotakiwa na kuongeza kuwa Matarajio ni kuona tunatumia chumvi yetu ya ndani yenye ubora unaotakiwa ili kuwanufaisha wazalishaji wetu.

Sambamba na hilo, Waziri Mavunde ameitaka STAMICO kuangalia uwezekano wa kuingia mikataba ya utatu kati yake, wazalishaji hao wa chumvi pamoja na mabenki ili wazalishaji wawezeshwe kupata mikopo nafuu hatimaye wazalishe chumvi ya kutosha na kutosheleza uhitaji.

Awali, akitoa taarifa fupi kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO,Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa Chimbuko la Mradi huo ni Maendeleo ya utekelezaji wa mipango ya Shirika pamoja na Maagizo ya Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza kusaidia wachimbaji wadogo wakiwemo wa chumvi.

Dkt. Mwasse amesema kuwa mbali na Kiwanda hicho kuchenjua madini ya chumvi, pia kitakuwa kinatoa Shamba darasa kwa wakulima wa chumvi ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha chumvi yenye ubora zaidi na pia kitatoa uhakika wa soko kwa wakulima wa chumvi nchini huku akibainisha kuwa chumvi itakayotoka katika kiwanda hicho itakuwa na ubora wa asilimia 99.5 inayohitajika duniani kote.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo alieleza kwamba mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho unataraji kukamilika na kuanza uzalishaji Mwezi Aprili, 2025 na kubainisha kuwa tayari mtambo umeshaagizwa kutoka nchini India na kulipiwa asilimia 50 ya gharama, na unatarajiwa kuwasili mwezi Oktoba, 2024.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Lindi, Mhe. Zainab Telack amesema kuwa, kukamilika kwa kiwanda hicho kutasaidia kufungua fursa sio tu kwa wakulima wa chumvi, bali kwa wananchi wa mkoa huo na kwamba kwa uzoefu wa STAMICO ana uhakika ujenzi utakamilika kwa wakati na kutimiza ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wazalishaji wa chumvi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news