JAKARTA-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) iko tayari kushirikiana na Shirika la Pelindo kujenga Bandari Jumuishi ya Mangapwani.
Ni bandari ambayo itajumuisha sehemu ya kuhifadhi nafaka, makontena, bandari kavu, chelezo pamoja na hifadhi ya mafuta.Pia, bandari hiyo Jumuishi ya Mangapwani inalenga kuwa kituo cha kuhudumia eneo la Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ijulikanayo kama Trans-shipment Port.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 5,2024 alipotembelea Bandari ya Tanjung Priok iliyopo jijini Jakarta, Indonesia na kukutana na uongozi wa Shirika la Pelindo linalomilikiwa na Serikali ya Indonesia ambalo linaendesha shughuli zote za bandari nchini humo.
Rais Dkt. Mwinyi amesema, anatambua kuwa Indonesia na Zanzibar zinafanana kwa kuwa ni nchi za visiwa na hutegemea bahari kwa shughuli za usafirishaji.
Aidha, amesema muundo huo wa kijiografia wa visiwa una changamoto mbalimbali za usafirishaji, hivyo bandari inachukua nafasi muhimu katika kutatua changamoto za kibiashara pamoja na kuchochea kupanda kwa uchumi wa nchi.
Naye Bw. Arif Suhartono ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Pelindo ambalo lina matawi 71 nchini humo likijumuisha kisiwa cha Sumatra kwa upande wa Magharibi hadi Mashariki ya Papua amesema,ziara hii iwe mwanzo wa ushirikiano wa karibu zaidi na kuweka misingi ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Indonesia na Zanzibar.