Benki Kuu za Afrika zajadili matumizi ya Akili Mnemba (AI)

PORT LUIS-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ameungana na magavana wa nchi mbalimbali za Afrika katika Mkutano wa mwaka wa 46 ya Umoja wa Magavana, kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili benki hizo pamoja na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kutekeleza majukumu yao.
Mkutano wa mwaka huu umefanyika katika visiwa vya Mauritius tarehe 3 hadi 4 Septemba 2024 ambapo, ulitanguliwa na kongamano maalum lenye kauli mbiu ya “Matumizi ya teknolojia ya uchambuzi wa Data nyingi (big data analytics), riba ya benki kuu na akili mnemba katika kukabiliana na mfumuko wa bei”.

Akizungumza katika moja ya mijadala ya mkutano huo, Gavana Tutuba alisema teknolojia ya uchambuzi wa data nyingi na akili mnemba ni muhimu sana katika kufanya uchambuzi na maamuzi ya kisera.

Alieleza kuwa teknolojia hiyo inafaa hasa katika mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba ya Benki Kuu ambao unatumiwa na nchi nyingi kutokana na uwezo wake katika kufanya maoteo ya mfumuko wa bei na viashiria mbalimbali vya kiuchumi.

Bw. Tutuba alisema hayo wakati akiongoza mjadala kuhusu “Faida na changamoto zitokanazo na matumizi ya teknolojia ya uchambuzi wa data nyingi na akili mnemba katika kufanya maoteo ya mfumuko wa bei na Utekelezaji wa Sera ya Fedha.”

Aliwaasa magavana wenzake, “kutumia teknolojia hizi kwa umakini ili kuepuka madhara yanayoweza kuambatana na tatizo la usahihi wa takwimu husika.”

Mada nyingine zilizojadiliwa katika mkutano huo ni matumizi ya riba ya benki kuu katika kukabiliana na mfumuko wa bei na athari zake katika uthabiti wa sekta ya fedha na maendeleo katika teknolojia ya huduma za fedha na akili mnemba yanavyoweza kutumika katika kukabiliana na mfumuko wa bei.

Magavana hao wa benki kuu barani Afrika walibadilishana mawazo kuhusu maendeleo katika teknolojia ya uchambuzi wa data nyingi na jinsi yanavyoleta mapinduzi katika ufuatiliaji wa mienendo ya viashiria mbalimbali vya kiuchumi na kufanya maamuzi usahihi ya kisera na kwa wakati.

Aidha, wamejadiliana kuhusu namna akili mnemba inavyoweza kuongeza usahihi katika kufanya maoteo na makadirio ya mfumuko wa bei na hivyo kuwezesha watunga sera kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati pamoja na changamoto zinazoambatana na matumizi ya teknolojia hiyo.

Changamoto zinajitokeza ni pamoja na usahihi wa takwimu kutokana na vyanzo vingi vya takwimu vikiwemo vilivyo rasmi na visivyo rasmi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii katika kutoa taarifa.

Hali hii, walisema, inahitaji umakini mkubwa namna ya kuzitumia data husika katika kufanya maamuzi.

Viongozi hao walibainisha changamoto nyingine kuwa ni gharama kubwa zinazoambatana na uwekaji katika mifumo ya kompyuta ili kuweza kufanya uchambuzi husika.

Pamoja na changamoto zilizotanabaishwa, washiriki wa kongamano hilo waliona kuwa faida za kutumia akili mnemba ni nyingi na hivyo kuna umuhimu kwa benki kuu barani Afrika kuanza kujipanga na kuwekeza katika matumizi ya teknolojia hiyo.

Mapema, akizungumza katika kongamano hilo la 46 la AACB, Waziri Mkuu wa Mauritius, Mhe. Pravind Kumar Jagnauth, amewataka Magavana wa benki kuu barani Afrika kushirikiana katika kuziongoza taasisi hizo ili kuhakikisha kuwa zinafanya kazi kwa weledi na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea hivi sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news