BMH yaja na Samia Mobile Surgical Camp, madaktari bingwa kufika mikoa ya pembezoni

DODOMA-Kwa sasa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inaanza kutoa huduma ya upasuaji wa Ubingwa wa juu hata kwa wananchi waliopo mikoa ya pembezoni baada kuzinduliwa kwa Samia Mobile Surgical Camp inayotumia magari yenye vyumba vya upasuaji, Ijumaa iliyopita.
Samia Mobile Surgical Camp inawezeshwa na magari maalumu yenye Teknolojia ya kisasa ya vyumba vya upasuaji, Wodi, vyumba vya kulala Watalaamu, umeme wa jua na mtambo wa kusafisha maji yaliyotolewa na Shirika la kujitolewa la SOTAC kutoka Uholanzi kwa ushirikiano wa BMH, ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi, na Wizara ya Afya.

Akizundua magari hayo Ijumaa iliyopita, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, amesema magari hayo maalumu yanadhihirisha dhamira aliyonayo Rais Samia kufikisha huduma za kibingwa na ubingwa wa juu kwa wananchi waliopo pembezoni mwa nchi na jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais amefungua Diplomasia ya Kimataifa na hata kugusa eneo la huduma za afya.

"Magari haya yatawawezesha Madkatari Bingwa wetu kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kufanya huduma ya upasuaji sehemu mbalimbali za nchi," amesema Waziri wa Afya wakati wa uzinduzi ambapo pia alipongeza sana ubunifu huu uliofanywa na Menejimenti BMH kwa kushirikiana na Balozi Chipeta nchini Uholanzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, amesema takribani wananchi 8000 wa sehemu mbalimbali za nchi watafikiwa kupitia huduma hiyo ya kliniki tembezi.

"Kupitia magari haya tutaweza kufanya huduma za upasuaji sehemu mbalimbali za nchi ikiwemo Pemba na Unguja, Wilaya za Dodoma, Kigoma na nchi ya jirani ya Burundi (ambapo tiba utalii itakuwa sehemu ya huduma hiyo) amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali.

Kwa upande wake, mwakilishi wa SOTAC, Bi Suzanne Hols, ameshukuru ushirikiano kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Shirika la SOTAC.

"Ushirikiano wetu na Hospitali ya Benjamin Mkapa ni mkubwa sana. Tuna miundombinu ya kuwawezesha kutoa huduma sehemu ambayo ni mbali na BMH. Tunadhamiria kuendelea kufanya kazi pamoja na BMH," alihitimisha Bi Suzanne.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news