DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iko mbioni kuandaa mwongozo utakaoainisha utaratibu wa kufuatwa katika kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha.


Bw. Nyanzowa amesema mapendekezo na maoni mbalimbali yaliyotolewa katika warsha hiyo yataisaidia BoT kutengeneza mwongozo utakaohakikisha malalamiko ya watumiaji wa huduma hizo yanashughulikiwa na kutatuliwa kwa ufanisi.
“Maoni na mapendekezo yaliyotolewa katika warsha hii yatakuwa ni sehemu muhimu katika mwongozo utakaotengenezwa na Benki Kuu ambao una lengo la kuboresha mchakato wa kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha kwa ajili ya kuongeza imani ya watumiaji wa huduma hizo,” amesema.
Aidha, ameziasa benki kuendelea kuimarisha michakato na taratibu za ndani za kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha huku zikihakikishi taratibu hizo zinaendana na miongozo mbalimbali inayotolewa na BoT.
“Huku BoT ikiendelea kutoa miongozo mbalimbali ya kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha, ni muhimu kwa taasisi zinazotoa huduma hizo kuzingatia miongozo hiyo,” amesema.
Pia, amesema watoa huduma za fedha wanaweza kutumia malalamiko hayo kama fursa ya kuboresha huduma na bidhaa zao na hatimaye kuleta utulivu katika sekta ya fedha.
“Kwa kutazama malalamiko kuwa ni fursa ya kuboresha na kukua, badala ya kuwa ni kikwazo, watoa huduma za fedha wanaweza kupunguza vihatarishi, kujenga imani pamoja na kuleta utulivu katika sekta ya fedha kiujumla,” Bw. Nyanzowa amesema.

Warsha hiyo, inayofanyika katika ofisi za BoT Dar es Salaam inatarajia kufikia tamati tarehe 20 Septemba, 2024, kwa ushiriki wa watoa huduma za fedha wasiokuwa mabenki.