DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha warsha kwa watoa huduma ndogo za fedha kuhusu namna bora ya kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma na bidhaa za kifedha nchini. Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo, Mkurugenzi wa Huduma Jumuishi za Fedha, Bw. Kennedy Komba, amesema utatuzi wa malalamiko ya wateja kwa ufanisi unawapelekea wateja kuwa na imani na huduma na bidhaa zinazotolewa na taasisi mbalimbali za fedha na hatimaye kuimarisha sekta nzima kwa ujumla.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa utatuzi wa malalamiko ni sehemu ya kulinda haki za mtumiaji wa huduma za fedha na inasaidia kurekebisha mapungufu yaliyopo katika utoaji huduma za kifedha pamoja na kuboresha sifa ya watoa huduma hao kwa wateja wao.
“Hii inalinda haki za watumiaji wa huduma za kifedha, pia, inasaidia kurekebisha mapungufu na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo na kuwaongezea sifa watoa huduma za kifedha,” amesema.
“Michakato imara ya utatuzi wa migogoro ya ndani (Internal Dispute Resolution) si tu inajenga uaminifu bali pia inatoa taarifa muhimu kwa wasimamizi wa sekta hiyo ili kuwasaidia katika utengenezaji wa sera kulingana na changamoto zilizopo,” amesisitiza Bw. Komba.
Pia, amewaambia kuwa ni muhimu kutambua jitihada zinazofanywa na Benki Kuu za kutengeneza Mfumo wa Utatuzi wa Malalamiko ya Kifedha (Financial Complaints Resolution System) na miongozo mbalimbali inayotolewa kwa ajili ya kuimarisha sekta ya fedha.
‘’Ni muhimu kutambua jitihada zinazofanywa na Benki Kuu za kuunda Mfumo wa Utatuzi wa Malalamiko ya Kifedha (FCRS) na mwongozo kwa ajili ya kushughulikia malalamiko katika sekta ya fedha. Mfumo huu utasaidia kuhakikisha malalamiko ya wateja yanatatuliwa kwa ufanisi, uwazi na usawa,” amesema.
Nao, washiriki wa warsha hiyo, wameishukuru Benki Kuu kwa kuandaa warsha hiyo na wameipongeza kwa kuzingatia usawa na kuhusisha pande zote mbili yaani watoa huduma za kifedha pamoja na watumiaji wa huduma hizo katika kutatua malalamiko ya wateja.
Warsha hiyo, inatarajia kufikia tamati tarehe 20 Septemba 2024 ambapo itahusisha pia washiriki kutoka kwenye mabenki na watoa huduma za malipo wasiokuwa mabenki (non-bank service providers).